Imam Alala Uddin Akongi na msaidizi wake waliuawa wakati wakitoka msikitini. |
Imamu mmoja na msaidizi wake wameuawa kwa kupigwa risasi
wakati wakitembea kuelekea nyumbani baada ya kushiriki ibada ya swala ya
Adhuhuri kwenye msikiti mmoja mjini New York.
Watu hao wamepigwa risasi kichwani kwenye eneo la Ozone
Park, hatua chache kutoka Al-Furqan Jame Masjid, kwa mujibu wa mashuhuda na
mamlaka za serikali.
Imam Alala Uddin Akongi ni kiongozi wa kidini
aliyeheshimika sana tangu alipowasili katika mji huo akitokea Bangladesh miaka
miwili iliyopita.
Msaidizi wake, Thara Uddin mwenye umri wa miaka 64, alijeruhiwa
vibaya sana na baadaye kufariki dunia baada ya kufikishwa hospitali.
Wote wawili walikuwa wamevaa mavazi ya Kiislamu
waliposhambuliwa, na waumini wa msikiti huo wamelaani shambulizi hilo na
kulitaja kuwa ni uhalifu wa chuki.
Mshambuliaji aliwafyatulia risasi kichwani akiwa karibu
yao na kisha akaondoka eneo hilo kwa miguu.
“Marekani haiku hivyo,” alisema mkazi mmoja wa eneo
hilo, Khairul Islam, mwenye umri wa miaka 33. “Tunamlaumu Donald Trump kwa hili
... Trump na maigizo yake ndio ametengeneza Islamophobia (chuki dhidi ya
Uislamu).”
Polisi wanasema kuwa waliitikia ripoti za tukio hilo saa
8:00 mchana kwa majira ya New York.
Idadi kubwa ya Waislamu walikusanyika kwenye eneo la
mauaji hayo, huku wakiliaani tukio hilo linalodhihirisha uhalifu wa chuki.
Kampeni ya mgombea wa Urais wa Marekani kupitia chama
cha Republican imekuwa ikitawaliwa na kauli tata dhidi ya jamii za watu
wachache wanaoishi nchini humo. Kauli zake zinawajumuisha kuwapiga marufuku
Waislamu wote wasiingiea Marekani na kuwafukuza wahamiaji wa Kimexico kwa
kujenga ukuta mrefu kwenye mpaka wa Marekani na Mexico.
Aidha, amekuwa akisema kuwa ataweka hifadhidata maalumu
ya kuwafuatilia Waislamu wote na kwamba Marekani haitakuwa na chaguo jingine
bali kuifunga misikiti yote.
Wazo la Trump limelaaniwa na Wasialmu, makundi ya haki
za binadamu na Chama cha Democratic, huku wapinzani wake ndani ya chama chake
cha Republican wakizielezea hatua hizo kuwa zitasababisha mfarakano, hazina
tija na ni kinyume na tunu za Marekani.
Ungana nasi kupitia WhatsApp: +255 712 566 595
0 comments:
Post a Comment