![]() |
| Wananchi mbalimbali, wakiwemo wanasheria na wanaharakati wa taasisi za kiraia, wakiandamana mjini Nairobi Julai 4, 2016 kupinga mateso na mauaji ya kiholela ya raia watatu yanayodaiwa kufanywa na maafisa wa jeshi la polisi. |
Mamia ya Wakenya wameandamana katika mji mkuu wa Kenya,
Nairobi, wakipinga kile walichokiita kuwa ni mauaji ya kiholela dhidi ya wakili
maarufu na mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu.
Waandamanaji walipita katika mitaa ya Nairobi wakiwa
wamebeba mabango yanayomtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Joseph Nkaissery,
ajiuzulu kufuatia kifo cha Willie Kimani, mteja wake na dereva wao, ambacho waandamanaji
hao walidai kuwa kilifanywa na polisi.
Baadhi ya waandamanaji walibeba jeneza lililoandikwa
maneno yasemayo “Komesha mauaji ya kiholela” wakati wengine walivaa fulana
zenye kauli mbiu isemayo “Komesha mauaji yanayofanywa na polisi.”
Miili ya Kimani, mteja wake Josephat Mwendwa dereva
taksi Joseph Muiruri iliokotwa wiki iliyopita. Watatu hao walitoweka baada ya
kutoka mahakamani mnamo Juni 23.
Mamlaka zinasema kuwa mikono ya Kimani ilikuwa imefungwa
na kamba, vidole vitatu vilikuwa vimekatwa na macho yake yalikuwa yameng’olewa
pindi miili ya watatu hao ilipookotwa kwenye ukingo wa mto mjini Nairobi siku
ya Ijumaa.
![]() |
| Picha ya maktaba ikimuonesha mwanasheria aliyeuawa Willie Kimani. |
Kimani na Muiruri walikuwa wakifanya kazi na shirika
moja la kimataifa la utetezi wa haki za binadamu wakati Mwendwa alikuwa ameishitaki
polisi mahakamani kwa madai ya kumfyatulia risasi na kumjeruhi.
Wanaharakati wanasema kuwa Kimani alikuwa akimtetea Mwendwa
dhidi ya mashitaka yaliyotolewa dhidi yake, ikiwa ni pamoja na umiliki wa
madawa ya kulevya na makosa mengine.
Polisi ya Kenya inasema kuwa itafanya uchunguzi kama
kuna askari yeyote aliyevunja sheria.
Maofisa watatu wamekamatwa kuhusu mauaji hayo, polisi
wamesema jana Jumamosi.
Wakenya wanalalamika kuhusu ufisadi wa polisi na
ongezeko la dhulma za polisi huku makundi ya kutetea haki za binadamu
yakizituhumu idara za polisi kuhusika na mauaji ya kiholela.
Mara kwa mara Kimani alikuwa mkosoaji mkubwa dhidi ya
dhulma za polisi.
![]() |
| Mamia ya Wakenya, wakiwemo wanaharakati wa haki za binadamu, mawakili na madereva wa taksi, wakifanya maandamano ya amani mjini Nairobi , Kenya, Julai 4, 2016, dhidi ya mauaji na utowekaji wa watu unaohusishwa na jeshi la polisi. |
Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu nchini humo imetoa
wito wa kufanyika kwa uchunguzi wa mauaji hayo, huku wanaharakati wengine
wakipinga madai ya polisi kwamba tukio hilo ni “kadhia iliyofanywa na maafisa
wachache waovu”.
“Wakenya wengi wamekuwa wakipotea, na hii ni hali
isiyovumilika hata kidogo,” mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria nchini humo, Isaac
Okero, alisema na kuitaka serikali kuchukua hatua.
Wakati huo huo, mapema leo, Shirika la kimataifa la
kutetea haki za binadamu, Amnesty International limetoa taarifa iliyokosoa
utekaji na mauaji ya watu hao watatu.
“Utekaji huu wa kushtusha, kutoweka na kuuawa kwa wakili
Willie Kimani, mteja wake na dereva wake… linapaswa kuwa indhari ya hali ya
haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Kenya,” lilisema shirika hilo.
Nalo shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali ya
Kenya kufanya uchunguzi wa kina kuhusu kadhia hiyo likisema kuwa “matukio ya
mauaji yanayofanywa na polisi yanaibuka kutoka maeneo mengi ya nchi kila mwaka.”
Kupata taarifa kupitia WhatsApp jiandikishe kupitia: +255 712 566 595



0 comments:
Post a Comment