| Picha ya gari linalodaiwa kuparamia watu. |
Kwa uchache watu 84 wamepoteza maisha na wengine 50
kujeruhiwa baada ya lori kuparamia kundi la watu waliokuwa wakisherehekea Siku
ya Taifa, katika mji wa Nice kusini mwa Ufaransa.
Lori hilo liliwavamia watu katika mji huo wakati wa
kurusha fataki. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi hiyo, Pierre-Henry
Brandet amesema kuwa watu 18 wapo katika hali mbaya.
Mie wa mji wa Nice, Christian Estrosi, ambaye
alihudhuria sherehe hizo wakati wa tukio hilo, aliandika kwenye mtandao wa
twitter: “Wapendwa wananchi wa Nice, dereva wa gari amesababisha vifo vya
makumi ya watu. Kwa sasa kaeni majumbani mwenu.”
Estosi alilielezea tukio
hilo kama “msiba mbaya kabisa katika historia ya Nice.”
Kiongozi huyo alinukuliwa akisema kuwa silaha na mabomu
vilikutwa ndani ya gari hilo baada ya dereva wa gari hilo kupigwa risasi na
kuuawa.
| Madaktari wakiwahudumia waathirika wa shambulizi la Nice, kusini mwa Ufaransa Julai 14, 2016. |
Shirika la habari la AFP limenukuu duru za polisi zikisema kuwa
dereva huyo ametambuliwa kama mwanaume mwenye umri wa miaka 31 mwenye asili ya Tunisia.
Picha iliyochapishwa kwenye mtandao wa Twitter imeonesha lori
jeupe likisimama katikati ya umati huku
upande wake wa mbele ukiwa umeharibiwa vibaya sana. Maofisi 4 wa polisi
walionekana wakijikinga nyuma ya mtende.
Picha nyingine iliwaonesha makumi ya watu wakiwa wamelala
barabarani baada ya shambulizi hilo. Aidha, video zilizorushwa kwenye mitandao
ya kijamii ziliwaonesha watu wakiwa wanakimbia barabarani katika hali ya
kuhamaki.
Kuna ripoti kwamba kulikuwa na makabiliano ya risasi kati ya
vikosi vya usalama na waliokuwa kwenye lori hilo, lakini hazijathibitishwa.
‘NI SHAMBULIZI LA KIGAIDI?’
Wakati huo huo, Rais Francois Hollande, aliyekuwa katika mji wa
Avignon, kusini mashariki mwa nchi hiyo, alirejea mjini Paris kushiriki vikao
vya kujadili shambulizi hilo kwenye Wizara ya Mambo ya Ndani.
Baadaye katika taarifa za moja kwa moja kwenye vyombo vya
habari, Rais huyo alisema kuwa shambulizi la mjini Nice lina “viashiria vya
ugaidi”.
"Hakuna kitakachotufanya tuvunjike moyo katika kupambana na
ugaidi. Tutaimarisha harakati zetu nchini Iraq na Syria. Tunaendelea
kuwashambulia wale wanaotushambulia kwenye ardhi yetu wenyewe,” alisema
akikusudia kundi la Daesh (IS).
![]() |
| Miili ikionekana chini baada ya shambulizi ya mji wa Nice. |
Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa idara ya
uchunguzi dhidi ya vitendo vya kigaidi imepewa jukumu la kufanya uchunguzi
kuhusu shambulizi la lori mjini Nice.
Japokuwa hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulizi
hilo, wafuasi wa kundi la Daesh (IS) waliripotiwa kusherehekea shambulizi hilo
kwenye mitandao ya kijamii.
Shambulizi hilo limetokea saa chache tu baada ya Hollande
kusema kuwa nchi hiyo haitaongeza muda wa hali ya hatari iliyowekwa kufuatia mashambulizi
mabaya ya kigaidi ya mwezi Novemba mwaka jana yaliyofanywa na kundi la Daesh
ndani na nje ya mji wa Paris.
(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kupitia: +255 712 566 595)

0 comments:
Post a Comment