![]() |
| Wakimbizi wa Sudan Kusini |
Siku nne za mapigano makali katika mji mkuu wa Sudan
Kusini, Juba, yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 300 na kuwalazimisha maelfu
ya watu kukimbia, Umoja wa Mataifa umesema.
Msemaji wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tarik
Jasarevic, amesema kuwa “ni zaidi ya vifo 300” tangu Julai 8.
Hata hivyo, Jasarevic amesema kuwa shirika hilo la UN
halina idadi kamili ya majeruhi.
Wakati huo huo, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa
limesema kuwa ghasia hizo za siku nne zimesababisha watu "42,000 kuwa
wakimbizi wa ndani” nchini humo.
"Idadi ya wakimbizi waliokimbilia katika nchi
jirani sasa imefikia watu 835,000," msemaji wa UNHCR William Spindler
amesema.
![]() |
| Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir (kushoto), akizungumza na vyombo vya habari Julai 14, 2016 katika ikulu ya Juba. Kulia ni mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika na Rais mstaafu wa Mali Alpha Oumar Konare. |
Wimbi jipya la mgogoro limeikumba Sudan Kusini ndani ya
siku kadhaa zilizopita.
Mapigano yalizuka mnamo Julai 8 karibu na ikulu mjini Juba,
ambapo Rais Salva Kiir na Makamu wa Kwanza wa Rais Riek Machar walikuwa
wamekutana kwa ajili ya mazungumzo.
Mapigano hayo yameirejesha nchi hiyo katika machafuko
mapya baada ya kuwa katika kipindi cha usitishaji mapigano kwa miezi kadhaa.
Shirika la Kimataifa la Wahamiaji (IOM) limesema kuwa
watu wengi walikuwa wakirudi nchini humo tangu makubaliano ya usitishaji
mapigano ulipoanza kutekelezwa.
John McCue, mkuu wa operesheni za IOM nchini humo,
amesema “huduma za kiutu kwa watu walioathiriwa zimeboreka sana tangu Jumatatu
(Julai 11). Lakini hali hiyo itaendelea iwapo usitishaji mapigano utatekelezwa.”
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka Sudan mwaka 2011.
Tangu wakati huo nchi hiyo imekuwa katika machafuko.
Mzozo huo umeibua migawanyiko mikubwa ya kikabila. Uliibuka
baada ya vita vya kugombania madaraka baina ya Rais Kiir kutoka kabila la Dinka,
na kiongozi wa waasi Machar kutoka kabila la Nuer.
Hatimaye pande hizo mbili zilisaini mkataba wa amani
mwezi Agosti 2015 kwa lengo la kuhitimisha mzozo huo.
Licha ya mkataba huo, mapigano yameendelea kushuhudiwa
nchini humo.
(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kupitia: +255 712 566 595)


0 comments:
Post a Comment