
Serikali ya Marekani imepiga marufuku ndege zote za nchi
hiyo kufanya safari kati yake na Uturuki baada ya jaribio la mapinduzi
lililotibuliwa kuikumba nchi hiyo na kusababisha ghasia.
Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini humo (FAA), ambayo
husimamia shughuli zote za usafiri wa ndege za nchi hiyo, imetoa taarifa kwa
ndege zote za kibiashara na za kibinafsi.
"FAA inafuatilia hali ya mambo nchini Uturuki kwa
kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Idara ya Usalama wa Ndani na itatoa
taarifa zaidi iwapo hali itaboreka,” ilisema katika taarifa yake.
Aidha, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani ilitoa
tahadhari kwa raia wa nchi hiyo kutosafiri kwenda Uturuki kufuatia jaribio la
mapinduzi lililosababisha vifo vya watu 265.
Jana Uturuki ilisema kuwa ilifanikiwa kuzima jaribio la
mapinduzi ya kijeshi lililofanywa na kikundi cha askari baada ya usiku uliojaa
milipuko, milio ya risasi na vifaru
vilivyokuwa vikizunguka katika mitaa ya mji mkuu Ankara, na mji mkubwa kabisa
nchini humo wa Istanbul.
Makabiliano makali yalilipuka kati ya vikosi vya jeshi
na askari walioshiriki katika mapinduzi hayo yaliyozimwa.
Mamlaka nchini Uturuki zilimnyooshea kidole cha lawama
mwanazuoni wa Kiislamu Fethullah Gulen anayeishi nchini Marekani kwamba alikuwa
nyuma ya tukio hilo na kutaka akabidhiwe kwa serikali ya Ankara.
Rais wa Uturuki Recept Tayyip Erdogan amesisitiza kuwa Washington
inapaswa kumkabidhi Gulen kwa serikali ya Ankara, akisema kuwa Uturuki
haijawahi kukataa ombi la Marekani la kuwakabidhi kwake washukiwa wa ugaidi.
Washington imesema kuwa italiangalia ombi hilo, huku
ikimtahadharisha mshirika wake huyo kutoka NATO kwamba kauli za wazi kwamba
Marekani ilihusika na njama hiyo ya mapinduzi
ni “uongo mkubwa” na zinaweza kuathiri uhusiano wa nchi hizo.
Jaribio hilo la mapinduzi lilitatiza operesheni za
kijeshi za Marekani nchini Iraq na Syria. Uturuki ilifunga anga yake dhidi ya
ndege za kijeshi na kuzima umeme kwenye kambi ya kijeshi ya Incirlik ambayo ni
kituo kikuu kinachotumiwa na ndege za Marekani katika kufanya mashambulizi
dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na kundi la Dola ya Kiislamu (Daesh).
(Tunaomba maoni yako kuhusu habari hii, na ungana nasi katika WhatsApp kupitia: +255 712 566 595)
0 comments:
Post a Comment