![]() |
| Wanajeshi wakiwa wameweka kizuizi kwenye daraja la Bosporus mjini Istanbul wakati wa jaribio la mapinduzi ya kuiangusha serikali usiku wa kuamkia leo. |
Kenan Evren, rais wa zamani wa Uturuki ambaye kwa sasa
anakabiliwa na mashitaka katika mahakama moja mjini Ankara, ndiye mtu wa hivi
karibuni kabisa katika msululu wa maafisa wa kijeshi walionyakua madaraka kwa
mapinduzi ya kijeshi.
Kwa muda mrefu jeshi limejichukulia kama “mlinzi wa demokrasia
ya Uturuki”, ambalo linaieleza kama dola kuu ya kisekula iliyoanzishwa na
Mustafa Kamal Ataturk, muasisi wa jamhuri ya sasa ya Uturuki. Limeingilia moja
kwa moja katika siasa za Uturuki, na mwaka 1997 lilifanya kile kinachoitwa na
wasomi kuwa ni “mapinduzi ya kisasa”.
MWAKA 1960
Mapinduzi ya kwanza katika jamhuri ya Uturuki yalitokea
mwaka 1960, wakati wa mvutano mkubwa kati ya serikali na upinzani.
Chama cha Kidemokrasia kilichokuwa kikitawala chini ya
uongozi wa Waziri Mkuu Adnan Menderes na Rais Celal Bayar, kilianza kuchukua
msimamo laini kwenye masuala ya dini yaliyokuwa yamezuiliwa na utawala wa muasisi
wa jamhuri hiyo, bwana Ataturk. Chama hicho kiliruhusu maelfu ya misikiti
kufunguliwa tena baada ya kufungwa, kikaruhusu adhana katika lugha ya Kiarabu
(badala ya Kituruki), na kufungua shule mpya kwa mafunzo ya kidini, pamoja na
mambo mengine ambayo awali yalikuwa yamezuiliwa. Pia chama hicho kilipunguza
muda wa lazima wa kuhudumu jeshini.
Wakati huo huo, chama hicho kiliingia katika mgogoro na
wapinzani kwa kuweka sheria kali za vyombo vya habari na hatimaye kuzuia
uchapishaji wa magazeti yenye ukosoaji.
Mivutano mikubwa ilisababisha serikali ya Menderes
kuweka sheria ya kijeshi mapema mwaka 1960. Jeshi liliingilia kati na
kuiangusha serikali mnamo Mei 27; rais, waziri mkuu na mawaziri kadhaa
walikamatwa na kushitakiwa kwa uhaini na makosa mengine. Menderes akanyongwa.
Jenerali Cemal Gursel alishika hatamu za madaraka – kama
rais na kama waziri mkuu kwa wakati mmoja – na huo ukawa mwanzo wa siasa zilizotawaliwa
na jeshi ambazo zilidumu mpaka mwaka 1965.
MWAKA 1971
Uchumi wa Uturuki ulidorora mwishoni mwa miaka ya 1960,
na anguko hilo la kiuchumi lilisababisha ghasia kubwa: vyama vya wafanyakazi vilifanya
maandamano ambayo wakati fulani yaligeuka kuwa ya fujo, na makundi ya mrengo wa
kulia yalishambuliana. Thamani ya sarafu ilianguka, mfumko wa bei wa kila mwaka
ulifikia asilimia 80.
Hivyo, mwezi Machi kwa mara nyingine jeshi liliingilia
kati katika juhudi za kurejesha mambo katika mkondo wake. Mkuu wa jeshi wakati
huo, jenerali Memduh Tagmac
alimpa waziri mkuu Suleyman Demirel mkataba wa makubaliano (memorandum).
Aliituhumu serikali yake kuipeleka nchi katika machafuko na kutaka kuundwa kwa “serikali
imara na inayoaminika kwa kufuata mawazo na mtazamo wa Ataturk.”
Saa chache baadaye Demirel
alijiuzulu baada ya kufanya kikao na baraza lake la mawaziri.
Katika kipindi hiki jeshi
halikutawala kwa njia ya moja kwa moja. Kwanza lilimtaka NIhat Erim wa chama
cha mrengo wa kulia cha Jamhuri ya Watu, kuunda serikali ya mpito ambayo
iliitawala mpaka mwaka 1973. Baada ya hapo bunge lilimtangaza Fahri Koruturk
(mwanajeshi mstaafu wa jeshi la wanamaji) kuwa rais wa nchi.
MWAKA 1980
Ukosefu wa uthabiti
uliendelea hata baada ya mapinduzi ya mwaka 1971: Uturuki ilibadilisha mawaziri
wakuu maara 11 katika miaka ya 1970, uchumi uliendelea kudorora, na makundi ya
mrego wa kushoto na wa kulia yaliendea kupambana mitaani. Maelfu ya watu
waliuawa.
Mwishoni mwa mwaka 1979, jeshi
lilianza kujadili uwezekano wa mapinduzi, na mwezi Machi mwaka 1980 kundi la
majenerali lilipendekeza kuchukuliwa kwa hatua. Hatua hiyo ilicheleweshwa mara
kadhaa, na hatimaye mwezi Septemba maafisa wa kijeshi walitangaza kwenye
televisheni ya serikali kuwa wameweka sheria ya kijeshi na kuivunja serikali.
Evren alichukua hatamu za
urais, na mwanajeshi wa jeshi la wanamaji, Bulend Ulusu akashika nafasi ya kuwa
waziri mkuu.
Miaka hii ya utawala wa
jeshi ilileta utulivu fulani nchini Uturuki. Mwaka 1983, Ulusu alirithiwa na
Turgut Ozal, ambaye kwa sasa anasifa sana kwa kuutuliza uchumi wa Uturuki kwa
kuvibinafsisha viwanda vingi vilivyokuwa vikimilikiwa na serikali. Mfumko wa bei
ulishuka na ajira zikaongezeka.
Aidha, jeshi liliwakamata
maelfu ya watu; watu kadhaa walinyongwa, huku wengine wengi wakiteswa au
kupotea tu.
Katiba mpya ilitengenezwa
na kupelekwa kwa wananchi kwa ajili ya kura ya maoni, ambapo ilipitishwa kwa
wingi.
MWAKA 1997
Uchaguzi wa mwaka 1995
ulikipa ushindi mkubwa chama cha Ustawi wa Kiislamu kilichoshika hatamu za
madaraka mwaka uliofuata na kuongoza serikali ya ushirika.
Hivyo, mwaka 1997 jeshi
lilitoa “mapendekezo” ambayo serikali haikuwa na jinsi zaidi ya kuyakubali. Waziri
Mkuu Necmettin Erbakan alikubali programu ya
elimu ya lazima ya miaka minane (iliyokusudia kuwazuia wanafunzi kujiunga
katika shule za kidini), marufuku ya hijabu kwenye vyuo vikuu, na hatua
nyingine. Kisha Erbakan alilazimishwa kujiuzulu.
Chama cha Ustawi kilifutwa
mwaka 1998, na Erbakan akapigwa marufuku kujihusisha na siasa kwa miaka mitano.
Baadhi ya wanachama wa
chama hicho, akiwemo rais wa sasa wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, waliamua
kuunda chama cha Haki na Maendeleo.
(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kwa: +255 712 566 595)
(Kupata habari kupitia WhatsApp, ungana nasi kwa: +255 712 566 595)

0 comments:
Post a Comment