
Uingereza imechagua kujiondoa kwenye Jumuiya ya Ulaya (EU)
baada ya zaidi ya asilimia 51 ya Waingereza kupiga kura ya kujiondoa kwenye
umoja huo wenye nchi wanachama 28 katika kura ya maoni ya kihistoria
iliyofanyika jana Juni 23.
Katika kura hiyo, wapiga kura wapatao asilimia 51.90 walihiari
kujiondoa EU, huku asilimia 48.10 wakipiga kura kubaki kwenye umoja huo.
Zaidi ya Waingereza milioni 17.4 walisema kuwa nchi hiyo
inatakiwa kuondoka kwenye jumuiya hiyo, huku wengine milioni 16.14 wakipendelea
kubaki katika EU.
London na Scotland ziliunga mkono kwa nguvu kura ya
kubaki katika EU ilhali Wales na maeneo mengine ya umoja wa Uingereza yakiwa na
watu wengi wanaounga mkono kura ya kujitoa.
Waungaji mkono wa kampeni ya “Kuondoka” walifurahia sana
matokeo yaliyoonesha kuwa wameshinda.
Kiongozi wa chama cha UK Independence Party, Nigel
Farage, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kushetehekea akisema kuwa nchi hiyo
ilikuwa inarudisha uhuru wake.
Watu waliopenda nchi hiyo kubaki katika jumuiya hiyo
walitoa hoja kwamba kuondoka itahatarisha ustawi wa Uingereza, kuua ushawishi
wake kwenye masuala ya kimataifa, na kusababisha vikwazo vya ufanyaji biashara
kati ya nchi yao na EU.
Kwa upande mwingine, wananchi waliounga mkono kura ya
kujitoa wanaamini kuwa Uingereza ikiwa nje ya umoja huo itaimarika katika
ufanyaji wa mazungumzo yake ya kibiashara, kuwa na udhibiti wa uhamiaji na kuwa
huru dhidi ya kile wanachoamini kuwa sheria nyingi za EU na urasimu uliozidi
kiwango.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron, ametangaza
kujiuzulu baada ya kura hiyo kutokana na mstakbali wake kama kiongozi kuwa
gizani.
Cameron, amesema kuwa ataachia ngazi mapema Oktoba pindi
chama chake cha kihafidhina kitakapofanya mkutano wake.
Waziri mkuu huyo amesema kuwa matakwa ya Waingereza
yanapaswa kuheshimiwa baada ya kuchagua kujiondoa EU.
Uamuzi huo umesababishwa fedha ya Uingereza kushuka. Paundi
imeporomoka vibaya sana dhidi ya dola ya Kimarekani, poromoko ambalo ni la aina
yake tangu mwaka 1985 huku masoko ya dunia yakitikisha kutokana na matokeo
hayo.
Suala la uanachama wa Jumuiya ya Ulaya limekuwa lenye
utata nchini Uingereza tangu ilipojiunga na Jumuiya hiyo ya kibiashara mwaka 1973.
Kura hiyo imesababisha radiamali ya viongozi mbalimbali
duniani, ambapo viongozi wengi wa EU walielezea wasiwasi wao juu ya hatua ya
Uingereza kujiondoa, huku wengine wakionya madhara ya kubaki katika jumuiya
hiyo.
0 comments:
Post a Comment