
Kwa uchache watu 36 wamepoteza maisha na wengine 147 kujeruhiwa
katika milipuko ya mabomu ya kujitoa mhanga na shambulizi la silaha za moto
katika uwanja mkuu wa ndege wa Istanbul, Atatürk airport, nchini Uturuki.
Baadhi ya safari za ndege zimeanza kurejea katika hali
ya kawaida huku baadhi zikifutwa au kuchelewa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na gavana wa Istanbul,
Vasip Şahin, tathmini inaonesha kuwa washambuliaji watatu wa kujitoa mhanga
walitekeleza mashambulizi hayo katika maeneo matatu tofauti ndani ya uwanja
huo.
Waziri Mkuu wa Uturuki, Binali Yıldırım, amesema kuwa
dalili za awali zinaonesha kuwa kundi la Daesh (IS) lilihusika na shambulizi
hilo lakini uchunguzi bado unaendelea.
Afisa mmoja wa afya amesema kuwa majeruhi sita wapo
katika hali mbaya.
Milipuko ilitokea kwenye lango la ndege za kimataifa,
ndege za ndani, na eneo la maegesho.
Waziri wa Sheria, Bekir Bozdağ, amesema kuwa mmoja wa
magaidi aliwafyatulia watu risasi kwa kutumia bunduki aina ya AK-47 na kisha
kujilipua.
Rais Recep Tayyip Erdogan ameitolea wito jumuiya ya
kimataifa kuunganisha nguvu katika kupambana na ugaidi, baada ya shambulizi
hilo la kigaidi, ambalo ni shambulizi la nne kufanywa mjini Istanbul ndani ya
mwaka huu pekee.
Uwanja wa ndege wa Atatürk ni miongoni mwa viwanja vya
ndege vyenye safari nyingi zaidi za ndege duniani, ambapo mwaka 2015 uliweza
kuwahudumia abiria zaidi ya milioni 60.
(Mzizima 24 WhatsApp: +255 712 566 595)
0 comments:
Post a Comment