![]() |
| Katika picha hii, kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un akishuhudia mazoezi ya kurusha kombora la masafa marefu katika eneo lisilojulikana, Machi 11, 2016 (Reuters) |
Korea ya Kusini imesema kuwa Korea ya Kaskazini
inaonekana kuwa imerusha kombora jingine baharini kwenye pwani yake ya mashariki
wakati ambapo mivutano inaendelea kwenye Peninsula hiyo ya Korea.
Wizara ya Ulinzi ya Korea ya Kusini imesema kuwa kombora
hilo linaonekana kutupwa leo kutokea mji wa Sondok.
Umbali na mtupo wa kombora hilo haivikuweza
kuthibitishwa mara moja, kwa mujibu wa afisa mmoja wa wizara hiyo.
Wakati huo huo, shirika la habari la Korea ya Kusini, Yonhap,
limesema kuwa kombora hilo linaonekana kuwa la masafa marefu.
‘Muungano’
dhidi ya Kaskazini
Tukio hilo linatokea katika kipindi ambacho Rais wa
Marekani Barack Obama akiwa ameitisha mkutano wa dunia juu ya usalama wa
nyuklia mjini Washington.
Pembezoni mwa mkutano huo, Obama ameungana na mwenzake
wa Korea Kusini Park Geun-hye, na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe, na kuahidi
kuongeza shinikizo dhidi ya Pyongyang kama jibu dhidi ya majaribio yake ya nyuklia
na makombora.
![]() |
| Rais Barack Obama (katikati) katika mkutano wa pande tatu pamoja na mwenzake wa Korea Kusini, Park Geun -hye (kushoto), na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe kwenye kilele cha mkutano wa usalama wa nyuklia mjini Washington, Machi 31, 2016. |
“Tumeungana katika juhudi zetu za kuzuia na kujilinda
dhidi ya uchokozi wa Korea Kaskazini,” Obama aliwaambia wanahabari kufuatia
mkutano huo wa pande tatu, ambao ulisisitiza haja ya jumuiya ya kimataifa
kuchukua hatua dhidi ya Pyongyang.
Mwezi uliopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
lenye wanachama 15 lilipitisha vikwazo vikali kabisa dhidi ya Korea Kaskazini. Vikwazo
hivyo vilipendekezwa na Marekani.
Suluhisho
la Kidiplomasia kwa suala la Korea
Wakati hayo yakitokea, wakati wa mkutano huo, Rais wa
China Xi Jinping ametoa wito wa kufanyika mazungumzo kwa lengo la kutatua
tatizo la Peninsula ya Korea.
“China iko tayari kufanya juhudi katika namna bora
kuanzisha mazungumzo yatakayozishirikisha pande sita,” shirika la habari la
China, Xinhua lilimnukuu Rais Xi akisema hapo jana wakati alipokutana na
mwenzake wa Korea ya Kusini mjini Washington.
![]() |
| Rais wa China, Xi Jingping akizungumza wakati wa mkutano na mwenzake wa Marekani, Barack Obama kwenye kilele cha mkutano wa usalama wa nyuklia mjini Washington, Machi 31, 2016. |
Mazungumzo ya pande sita aliyoyakusudia yanazihusisha
Urusi, China, Marekani, Japan, Korea ya Kusini na Korea ya Kaskazini. Mazungumzo
hayo yalikwama mwaka 2009 baada ya Umoja wa Mataifa kuiwekea Pyongyang vikwazo
vizito kwa kufanya majaribio ya silaha za nyuklia na makombora.
Wakati huo huo, vyombo vya habari vya Korea ya Kaskazini
viliuita mkutano huo wa masuala ya nyuklia kuwa ni wa “kipuuzi” kwa kuwa
unajaribu kukosoa kitu ambacho Korea ya Kaskazini inakiona kuwa ni “uhalali
wake wa kutumia silaha za nyuklia”.
Katika hatua nyingine, Muungano wa Ulaya umeongeza muda
wa vikwazo vya kibiashara na kifedha dhidi ya Korea Kaskazini.
Muungano huo wenye wanachama 28 umesema kuwa hatua hizo
mpya zimewekwa dhidi ya usafirishaji na uingizaji wa bidhaa zinazoweza kuongeza
uwezo wa vikosi vya jeshi la nchi hiyo.
Aidha, Muungano huo umeongeza vikwazo dhidi ya Korea ya
Kaskazini, ikiwa ni pamoja na kuzishikilia mali za serikali zenye uhusiano na programu
za nyuklia au makombora ya masafa marefu ya nchi hiyo.
Mivutano kati ya Korea hizo mbili imeongezeka tangu
mwanzoni mwa mwaka 2015 baada ya Kaskazini kufanya jaribio la nyuklia mwezi
januari na uzinduzi wa kombora la masafa marefu ililolifanya mwezi Februari.
Pyongyang ilisema kuwa urushaji wa kombora hilo ulilenga
kuweka satelaiti ya uchunguzi wa ardhi angani. Hata hivyo, Washington na Seoul zilikosoa
hatua hiyo na kusema kuwa ililenga kuficha ukweli kwamba ni jaribio la kombora
la masafa marefu.
Korea Kaskazini imeahidi kujenga ghala la nyuklia katika
juhudi za kujilinda dhidi ya jeshi la Marekani, ambalo mara kwa mara hutuma
meli za kivita zenye silaha za nyuklia na ndege zenye uwezo wa kubeba silaha za
atomiki kwenye eneo hilo.
Washington pia hufanya mazoezi ya kijeshi pamoja na
Korea Kusini, ambayo Korea ya Kaskazini inayaona kuwa ni maandalizi ya vita na
ni kitisho cha moja kwa moja dhidi ya usalama wake.
(WhatsApp: +255 763 348 213)



0 comments:
Post a Comment