![]() |
| Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas |
Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas, ameonya kuwa Mamlaka
ya Palestina iko “kwenye ukingo wa kuanguka” kutokana na utawala wa Israel
kuendelea na operesheni zake za kijeshi katika maeno ya Ukingo wa Magharibi ambayo
yapo chini ya utawala wake.
Katika mahojiano na Channel 2 ya Israel, Abbas alimtaka
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kukomesha uvamizi dhidi ya Wapalestina
katika eneo la Ukingo wa Magharibi na kusema kuwa katika tukio moja, vikosi vya
Israeli vilifika mpaka mlangoni kwake mjini Ramallah.
Kiongozi huyo alionya zaidi kuwa “intifada mbaya kabisa”
itaikumba Israel iwapo Tel Aviv itashindwa kukomesha operesheni zake za kijeshi
katika ardhi za Wapalestina.
Alilikosoa jeshi la Israeli kwa kukataa kushirikiana
taarifa za kiintelejensia kuhusu hatua inazozifanya katika maeneo ya
Wapalestina.
“Sasa mimi ninafanya nini hapa? … mnataka niwe
mfanyakazi wenu. Wakala wenu. Silikubali hili,” alisema.
Eneo la Ukanda wa Magharibi linalokaliwa kimabavu
limeshuhudia wimbi jipya la mivutano kati ya waandamanaji wa Kipalestina na
vikosi vya utawala wa Israeil tangu mwezi Oktoba mwaka jana.
Katika miezi ya hivi karibuni, vikosi vya Israeli
viliongeza kampeni yake ya kuwatia hofu Wapalestina, kwa kuzivamia nyumba zao
katika miji ya Ukanda wa Magharibi na kuwatia kizuizini wengi wao.
Aidha, Abbas aliituhumu Israel kwa kuendelea kukiuka
Mkataba wa Oslo kwa kuivamia miji ya Wapalestina bila kizuizi.
Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya Israel na Chama cha
Ukombozi wa Palestina (PLO) mwaka 1993 na 1995 kwa lengo la kutatua mgogoro wa
Wapalestina na Waisrael na kutekeleza haki ya Wapalestina kujiamulia mambo yao.
Hata hivyo, miongo miwili imepita tangu kusainiwa kwa
mikataba hiyo, ambapo makundi mengi ya Kipalestina yanasema kuwa mikataba hiyo
imekuwa ikitumiwa na Israel kuimarisha harakati za kuwakalia kimabavu na
kutenda jinai na uhalifu mwingi dhidi ya Wapalestina.
![]() |
| Askari wa Israel wakijiandaa kuuondosha mwili wa Mpalestina waliyemuua katika mji wa al-Khalil (Hebron) kwenye Ukanda wa Magharibi, Machi 24, 2016. |
Abbas aliendelea kusema kuwa anasikitishwa sana na video
mpya iliyorushwa ikimuonesha askari wa Israel akimuua Mpalestina aliyejeruhiwa.
Aliyaelezea mauaji hayo kama “ya kinyama” na kusema “kwa
bahati mbaya tunasoma radiamali na maandamano ndani ya Israel yanayopinga
askari huyo kufikishwa kizimbani, na yanayotetea asikamatwe. Maelezo kama hayo yanatukera
kwa kiasi kikubwa mno.”
Akielezea kuhusu madai ya mashambulizi ya Wapalestina
dhidi ya askari wa Israel, Abbas alisema “Jiulizeni kwa nini kijana wa miaka 15
anachukua kisu huku akijua kuwa anaenda kufa, na bado anaenda. Jiulizeni kwa
nini. Ni kwa sababu hana matumaini” ya kupata amani.
Zaidi ya Wapalestina 200 wameuawa na vikosi vya Israel
katika ghasi zinazoendelea sasa.
Umoja wa Mataifa na mashirika kadhaa ya haki za binadamu
yameikosoa Israel kwa kutumia nguvu iliyopitiliza, na kusema kuwa mauaji mengi
ni ya kiholela.
Pia wamelaani ukaliaji wa miongo mingi dhidi ya ardhi za
Wapalestina na kubainisha kuwa huo ndio mzizi wa ghasia zinazoendelea.
Wachunguzi wanasema kuwa utawala wa Israel unakabiliwa
na mkanganyiko wa Intifada (mwamko wa mapinduzi) ya Wapalestina, huku hatua
zinazochukuliwa na Tel Aviv kuzuia zikiwa zimeshindwa.
(WhatsApp: +255 763 348 213)


0 comments:
Post a Comment