
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) leo
tarehe 1/4/2016 imemfikisha Mahakamani Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa Mbunge
wa Sumwe ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Mtaji na Uwekezaji kwa kosa la
kushawishi na kuomba Rushwa ya Shilingi Milioni thelathini (30,000,000/-)
kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya mwaka 2007 kifungu
cha 15 (i)(a) na (2).
Akiwa kama mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji tarehe
13/3/2016 Mhe. Ndassa alimwomba rushwa ya shilingi Milioni 30 kutoka kwa
Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Felchesmi J. Mramba
ili amsaidie kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati Mtaji na Uwekezaji
kupitisha bila kipingamizi taarifa ya TANESCO kwa mwaka 2015/2016.
Mbunge huyo amefunguliwa kesi namba 118/2016 na
alisomewa mashtaka hayo na Wakili wa TAKUKURU Dennis Lekayo akishirikiana na
Emmanuel Jacob katika Mahakama ya Kisutu mbele ya Mhe. Hakimu Emirius Mchauro.
Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini
mmoja na kulipa shilingi milioni 10. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea
na kesi hii itatajwa tena tarehe 18/4/2016.
0 comments:
Post a Comment