SANTIAGO, Chile
Rais wa Brazil, Dilma Rousseff, anakabiliwa na shinikizo
kubwa la kisiasa baada ya vyama viwili vilivyokuwa washirika katika serikali
yake kusema kuwa vitapiga kura ya kutokuwa na imani naye ndani ya bunge.
Muungano wake unaoongozwa na Chama cha Wafanyakazi,
umebakiwa na Chama cha Maendeleo chenye wabunge 47 na chama cha Umma chenye
wabunge 22.
Rousseff anatuhumiwa kukiuka sheria za bajeti ili kuficha
matatizo ya kibajeti kuelekea uchaguzi wa urais uliofanyika mwaka 2014.
Mchakato huo wa kutengua urais wake unategemea uamuzi wa
bunge lenye wabunge 513 ambalo kesho litaanza kujadili iwapo liendelee na
mchakato huo au la.
Ili kusonga mbele, kutahitajika theluthi mbili ya kura
za wagunge 342 kwa ili hatua hiyo ifikishwe mbele ya bunge la Seneti.
Makamu wa Rais, Michel Temer, ambaye atachukua uongozi
wa nchi iwapo bunge la Seneti litapitisha uamuzi wa kutengua madaraka ya rais,
amesema kuwa amejiandaa kuchukua uongozi wa nchi iwapo Rousseff atang’olewa.
Kauli ya Temer inakuja siku moja baada ya hotuba yake
moja kuvuja mtandaoni ambapo alitangaza hatua kadhaa serikali ya mpito baada ya
rais kuondolewa.
Mapema jana Rais Rousseff alisema kuwa ameamua kupambana
mpaka dakika ya mwisho kwa ajili ya kuuokoa utawala wake.
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo,
mawaziri kadhaa wanakiri kuwa upo uwezekano wa kushindwa katika zoezi hilo
litakalofanyika Jumapili hii.
“Watu wote wanakubaliana kuwa serikali inakabiliwa na
wakati mgumu kabisa kuwahi kuikumba,” limeandika gazeti la Folha de Sao Paulo.
0 comments:
Post a Comment