| Viongozi mbalimbali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa mkutano wa umoja huo unaofanyika mjini Istanbul. |
ISTANBUL
Kilele cha 13 cha mkutano wa Jumuiya ya Ushirikiano wa
Kiislamu (OIC) kimeanza leo mjini Istanbul, nchini Utuurki.
Hii ni mara ya kwanza kwa Uturuki kuandaa mkutano huo wa
siku mbili tangu kuanzishwa kwa umoja huo mwaka 1969.
Wakati wa mkutano huo, Uturuki itachukua uenyekiti wa umoja
huo kwa kipindi cha miaka miwili. Mkutano huo unafanyika chini ya kauli mbiu
ya: “Umoja na Mshikamano kwa ajili ya Haki na Amani”.
Katika hatua ya ufunguzi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni
wa Misri, Samih Shukri anatarajiwa kutoa hotuba ya kwanza akiwakilisha taifa
lake ambalo liliandaa mkutano wa 12 wa OIC mwaka 2013.
Mkutano huo utaimarisha umoja na mshikamano baina ya
mataifa ya Kiislamu katika kupambana na ugaidi, kwa mujibu wa taarifa iliyowekwa
kwenye tovuti rasmi ya umoja huo.
Aidha, mkutano huo wa ngazi ya juu wa viongozi wa
Kiislamu unatarajiwa kujadili hali ya mambo katika mataifa ya Syria, Yemen,
Palestina, Iraq, na Azerbaijan. Azimio rasmi linatarajiwa kutolewa mwishoni mwa
mkutano huo.
OIC iliyoanzishwa mwaka 1969, ina mataifa wanachama 57
na kuwakilisha sauti ya pamoja ya Ulimwengu wa Kiislamu, kwa mujibu wa taarifa
hiyo.
Umoja huo unatajwa kuwa jumuiya ya pili kwa ukubwa
inayozijumuisha serikali baada ya Umoja wa Mataifa, na ulianzishwa mwishoni mwa
mkutano wa kihistoria uliofanyika katika mji mkuu wa Morocco, Rabat baada ya
shambulizi la kiuharibifu lililofanywa dhidi ya Msikiti wa Al-Aqsa mjini Jerusalem
mwaka 1969. Mataifa wanachama yamekuwa yakikutana mara moja kila baada ya miaka
miatatu, hasa kwa ajili ya kutathmini hali ya mambo katika nchi husika.
Morocco imewahi kuandaa mkutano huo mara tatu, Senegal mara
mbili na Saudi Arabia, Pakistan, Qatar, Kuwait, Iran, Malaysia na Misri mara
moja tangu 1969.
Kwa kawaida, mgogoro wa Israel na Palestina hutawala
agenda za mikutano hiyo, ikiwemo ile ya mwaka 1969 mjini Rabat, mwaka 1974 mjini
Lahore na ule wa mwaka 1981 uliofanyika mjini Makkah.
Mkutano wa mwaka 1981 mjini Makkah ulitathmini mgogoro
wa kisiasa na kiuchumi nchini Afghanistan na mzozo wa Iran na Iraq.
Katika mkutano uliofanyika mjini Casablanca mwaka 1984, viongozi
wa mataifa 42 wanachana wa umoja huo walisisitiza usitashaji mapigano kati ya
Iran na Iraq ambayo ni mataifa jirani.
Ukaliaji mabavu wa Israel dhidi ya ardhi ya Palestina
ilikuwa ajenda kuu katika mikutano iliyofanyika mwaka 1991 mjini Dakar,
Senegal, mwaka 2000 mjini Doha, Qatar, mwaka 2003 nchini Malaysia na ule wa
mwaka 2008 uliofanyika tena mjini Dakar.
Mkutano wa mwisho ulifanyika mjini Cairo nchini Misri
mwaka 2013, ambao ulijadili ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu mbali na suala
la ujenzi wa makazi ya Wayahudi kwenye ardhi za Wapalestina.
0 comments:
Post a Comment