![]() |
Rais Barack Obama (kulia) akizungumza pamoja na Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani kwenye mkutano na vyombo vya habari katika ikulu ya Marekani, mjini Washington DC, Machi 24, 2015. |
RAIS wa Marekani, Barack Obama, amezungumza na mwenzake
wa Afghanistan, Ashraf Ghani kuhusu mazungumzo ya amani na kundi la Taliban, na
kueleza uungazi mkono wa Washington kwenye mchakato huo wa maridhiano.
Kauli ya Obama imekuja baada ya maafisa wa Afghanistan, Marekani,
Pakistan na China kusema mwezi uliopita kuwa serikali ya Afghanistan na kundi
la Taliban walitarajiwa kuwa na mkutano wa moja kwa moja wa mazungumzo ya amani
ndani ya wiki ya kwanza ya mwezi Machi katika mji mkuu wa Pakistan.
Wakati akizungumza na Rais Ghani kwa njia ya video,
Obama alisisititza juu ya nafasi ya rais huyo wa Afghanistan katika kufanya
kazi na majirani wa nchi hiyo ili kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kusonga
mbele katika mchakato wa kufanya maridhiano na kundi la Taliban, taarifa ya
Ikulu ya Marekani imesema.
Aidha, Rais Obama alisisitiza uungaji mkono wa Marekani
kwenye mazungumzo ya amani yatakayopunguza ghasia na kuhakikisha amani ya kudumu
inapatikana nchini humo na katika ukanda huo, iliongeza taarifa hiyo.
Makamu wa Rais wa Marekani, Joe Biden na Afisa Mtendaji
Mkuu Abdullah Abdullah walihudhuria wakati wa mawasiliano hayo.
Ofisi ya Rais wa Afghanistan, imesema kuwa Obama
alivipongeza vikosi vya ulinzi vya Afghanistan kwa utendaji mzuri na ujasiri
katika kupambana na ugaidi.
“Rais Barack Obama alimweleza Rais Ghani kuwa anavutiwa
na utendaji na ujasiri wa vikosi vya ulinzi vya Afghanistan katika kupambana na
ugaidi,” ilisema ikulu ya Kabul.
Kwa mujibu wa ripoti moja ya Pentagon iliyotolewa mwezi
Januari, hali ya usalama nchini Afghanistan ilizorota katika nusu ya pili ya
mwaka 2015, kutokana na wapiganaji wa Kitaliban kufanya mashambulizi zaidi na
kusababisha hasara kubwa kwa vikosi vya serikali ya Afghanistan.
Afghanistan imekuwa katika vurugu na ghasia kwa zaidi ya
miaka 14 baada ya Marekani na washirika wake kuishambulia nchi hiyo kama sehemu
ya vita vya Washington dhidi ya ugaidi. Ingawa mashambulizi hayo ya mwaka 2001
yaliwaondosha madarakani Wataliban, maeneo mengi ya nchi hiyo bado yanakabiliwa
na ghasia na ukosefu wa usalama.
Licha ya Rais Obama hapo awali kuahidi kuwa mpaka
mwishoni mwa utawala wake atakuwa ameviondosha vikosi vyote vya Marekani,
alitangaza mipango ya kubakisha askari 5,500 nchini humo atakapoachia madaraka
mwaka 2017.
0 comments:
Post a Comment