
NI umafia wa aina yake uliofanikisha watuhumiwa watatu,
wakiwamo wa ujangili na mauaji kutoroka kwa kutoboa tundu kwenye ukuta wa Kituo
cha Polisi Wilaya ya Meatu mkoani Simiyu.
Watuhumiwa hao, wawili wa ujangili na mmoja wa mauaji,
walitoroka muda mchache baada ya kutoka mahakamani ambako walipelekwa kutokana
na kesi zilizokuwa zinawakabili.
Tukio hilo la aina yake lilitokea Februari 19, mwaka huu
saa nane usiku, ambapo inaelezwa kuwa watuhumiwa hao walitoroka wakati mvua
ikinyesha baada ya kutoboa ukuta na kitu chenye ncha kali.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Bariadi,
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Audax Majaliwa, alisema kutokana na
tukio hilo askari saba wanashikiliwa.
Alisema watuhumiwa hao kabla ya kutenda tukio hilo,
Februari Mosi mwaka huu, walifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya
Wilaya ya Meatu kwa ajili ya kusikiliza kesi zinazowakabili.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema baada ya kusikilizwa kwa
kesi zao, walirudishwa mahabusu katika kituo hicho cha polisi, wakisubiri
kukamilika kwa taratibu za kuhamishiwa katika gereza la wilaya.
Aliwataja watuhumiwa hao waliotoroka kuwa ni pamoja na
Chiluli Sitta (28) mkazi wa kijiji cha Mwasangula Kata ya Itinje wilayani humo,
ambaye alikuwa akikabiliwa na kesi a mauaji.
Wengine ni Msanja Ndangule (45) na mtoto wake Paschal
Masanja, wote wakazi wa Kijiji cha Sapa, Kata ya Itinje wilayani humo ambao
walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ujangili.
“ Watuhumiwa hawa walitumia sehemu ya bafu na choo
ambayo kwa kawaida inakuwa imeharibika au kuloana sana kutokana na mkojo ambao
ukojelewa na mahabusu.
“Kwa kawaida mkojo na simenti havipatani, tuna hofu kuwa
sehemu hiyo ilikuwa haina ugumu hata kidogo,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.
Alisema kuwa pamoja na ukuta huo kuonekana umeharibiwa
na mkojo hivyo kuwarahisishia watuhumiwa hao kutoboa na kutoroka, kulikuwa na
uzembe uliofanywa na askari waliokuwa zamu pamoja na mkuu wa kituo hicho.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema katika mahabusu hiyo
walikuwamo watuhumiwa sita, ambapo watatu walitoroka na wengine wawili
walibaki, ambao ndiyo walitoa taarifa kwa askari kuwa wenzao wametoroka kwa
kutoboa ukuta.
“Jambo la kushangaza kwanini wengine walibaki? Na hawa
waliotoroka wanatoka kata moja, tuna hofu hapa kuwa kulikuwepo na njama, lakini
kwa waliobaki walieleza kuwa waliona dalili mapema kwa wenzao kuwa wako kwenye
mipango mikubwa,” alisema Kaimu Kamanda Majaliwa.
Majaliwa alisema kuwa kutokana na tukio hilo tayari
jeshi hilo limeanza kuchukua hatua za haraka, ambapo mpaka sasa askari saba
wanashikiliwa ili kusaidia uchunguzi.
Aliwataja askari hao kuwa ni G. 8371 PC Adam, F. 9840 DC
Hussen, D. 5582 Koplo Peter ambaye alikuwa kiongozi wa zamu siku ya tukio, G.
4806 PC John, G.8602 PC Yassin, H. 8410 PC Hery na WP. 1125 Hadija.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema kuwa baada ya hatua hizo
kwa askari hao, taratibu nyingine za kushtakiwa kijeshi zitaendelea mara baada
ya uchunguzi kukamilika.
Alisema kuwa askari hao wanahusika moja kwa moja kwani
licha ya mvua kunyesha, walitakiwa kufanya kazi ya kulinda kituo hicho pamoja
na watuhumiwa hao, na kuongeza kuwa uchunguzi wa awali umeonyesha walikuwa
wamelala.
Kaimu Kamanda Majaliwa alisema hadi sasa watuhumiwa hao
hawajapatikana na msako mkali unaendelea wa kuwatafuta ili kurudishwa gerezani
kwa ajili ya kuendelea kusikiliza mashtaka yanayowakabili.
WAZIRI KITWANGA
Akizungumzia tukio hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani,
Charles Kitwanga, amesema ametuma timu ya uchunguzi wilayani Meatu ili kubaini
chanzo cha watuhumiwa hao kutoroka wakiwa chini ya ulinzi.
“Nawaomba muwe na subira, nimetuma timu ya wataalamu
wangu kwenda kuchunguza kwa kina sababu za watuhumiwa hawa kutoroka wakiwa
chini ya ulinzi…nitaujulisha umma baada ya kupokea ripoti.
“Naamini ripoti itakayokuja ndiyo itanipa picha halisi
ya tukio hili, maana najiuliza ilikuwaje watu watoroke wakati wanakabiliwa na
makosa mazito hivi,” alisema Waziri Kitwanga.
Alisema kutokana na hali hiyo, ametuma kikosi maalumu
cha makachero kwa ajili ya kuwasaka kwa udi na uvumba watuhumiwa wote.
CHANZO: Mtanzania
0 comments:
Post a Comment