
Rais wa Jamhuri ya Muungano John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza Makao
Makuu ya Benki Kuu ya Tanzania jijini Dar-es-Salaam ambapo pamoja na mambo
mbalimbali alitoa maagizo kadhaa yanayohitaji utekelezaji mara moja kwa
viongozi wa chombo hicho kikuu cha fedha nchini.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa
na Kaimu Mkurugenzi wa Habari wa Ikulu Bw. Gerson Msigwa Rais Magufuli
amemuagiza Gavana wa Benki Kuu kupitia ajira za watumishi wa taasisi hiyo na
kufanya upunguzaji wa watumishi hao hasa kama kazi zao zinaweza kufanywa na
watu wengine.
“Haiwezekani tukawa na kundi kubwa la wafanyakazi,
wanalipwa mishahara wakati hata kazi wanazofanya hazijulikani” amenukuliwa Rais
Magufuli katika taarifa hiyo ya Ikulu ambayo vyombo vya habari havikupewa
nafasi ya kuuliza maswali. Kwa mujibu wa taarifa hiyo Benki Kuu ya Tanzania ina
wafanyakazi wapatao 1391.
Pamoja na agizo hilo Rais Magufuli alitoa pia maagizo
mengine likiwemo lile la kutaka Benki hiyo isitishe mara moja malipo ya
malimbikizo ya madeni ambayo yanakaribia trilioni moja na ambayo tayari
yalikuwa yameidhinishwa kulipa. Taarifa hiyo imesema kuwa Rais ameagiza malipo
hayo yarejeshwe hazina kwa ajili ya kufanyiwa uhakika upya ili kujiridisha kuwa
wote ambao wameidhinishiwa kulipwa malipo hayo ni kweli wanastahili kiasi
kilichoidhinishwa. Hii ni mojawapo ya baadhi ya hatua za Rais Magufuli
kusimamia matumizi ya serikali na kudhibiti ubadhirifu.
Vile vile Rais Magufuli ameagiza kitendo cha madeni ya
nje ambacho awali kilikuwa Benki Kuu na
baadaye kuhamishiwa Wizara ya Fedha kirejeshwe tena Benki Kuu mara moja.
Taarifa hiyo imesema kuwa Rais ameagiza hilo ili “kuimarisha udhibiti wa
ukopaji na ulipaji wa madeni”.
Taarifa hiyo hata hivyo haikueleza kwanini uamuzi huu
umefanyika sasa na kama sababu zilizofanya kitengo hicho kiondolewe BoT
kupelekewa Wizara ya Fedha bado zipo au la. Kitengo cha madeni ya nje kilikuwa
maarufu sana miaka michache nyuma hasa kwa kuhusishwa na mojawapo ya kashfa
kubwa kabisa za fedha nchini – ile kashfa ya EPA. Ikulu haikutoa maelezo yoyote
juu ya uamuzi wa Rais na kesi za EPA ambazo hado hazijaisha au hata uchunguzi
ambao haujamalizika hasa kwa kampuni kama Kagoda ambayo ilidaiwa kuchota
mabilioni toka akaunti ya EPA.
CHANZO: Zama Mpya
0 comments:
Post a Comment