
MOSCOW: Watu wote 61 waliokuwa kwenye ndege ya Shirika
la Ndege la flydubai aina ya Boeing 737 wamepoteza maisha baada ya ndege yao
kupata ajali na kuteketea kabisa wakati ikitua katika mji wa Rostov-on-Don, kusini
mwa Urusi leo, maafisi wamesema.
Ajali hiyo imtokea wakati ndege hiyo ikijaribu kutua kwa
mara ya pili lakini hali mbaya ya hewa ilifanya ikosee njia na kulipuka.
“flydubai inasikitika kuthibitisha kuwa ndege namba FZ981
imepata ajali wakati ikitua na kwamba tukio hilo la kusikitisha limesababisha
vifo,” shirika hilo limesema kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Wizara ya mambo ya dharura nchini humo imethibitisha
kuwa abiria wote 55 na wafanyakazi 6 waliokuwa kwenye ndege wamepoteza maisha.
“Ndege aina ya Boeing 737 ilipata ajali wakati ikitua. Ilikuwa
imebeba watu 61. Wote wamepoteza maisha”, amesema msemaji wa wizara hiyo kama
alivyonukuliwa na shirika la habari la TASS.
Ndege hiyo iligonga chini mita mia moja kutoka eneo la
kutua wakati ikijaribu kutua kwa mara ya pili.
Picha za video kwenye vyombo vya habari vya eneo hilo
zimeonesha moto mkubwa ukiwaka kutoka kwenye eneo la ajali.
Mvua ilikuwa ikinyesha sana na tahadhari ya upepo mkali
ilikuwa imetolewa na wizara ya dharura ya eneo hilo, shirika la habari la TASS limesema.
0 comments:
Post a Comment