![]() |
Wafuasi wa kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye. |
Kiongozi machachari wa upinzani nchini Uganda, Kizza
Besigye, ametiwa nguvuni kwa mara ya nne ndani ya siku nane kufuatia uchaguzi
uliomrudisha madarakani Rais Yoweri
Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa muda mrefu.
Mapema leo polisi walisema kuwa wanaamini kuwa
kiongozi huyo wa upinzani alikuwa akijiandaa kuwaongoza wafuasi wake kwenda
ofisi za tume ya uchaguzi kuchukua matokeo rasmi bila kibali halali.
"Leo, [Besigye] aliratibu kundi la vijana
kwenda kuvamia tume ya uchaguzi. Tulikuwa na taarifa kuwa walikuwa wamepanga
kusababisha ghasia mjini,” msemaji wa polisi Patrick Onyango alisema.
Hata hivyo, kiongozi mwandamizi wa chama cha FDC cha
Besigye, alitoa wito wa kuachiliwa kwa kiongozi huyo, akisema kuwa amekataliwa
kukusanya ushahidi wa kupinga matokeo ya uchaguzi.
"Wanatakiwa kumuacha huru kwa sababu ana siku
14 tu za kupeleka pingamizi mahakamani. Amekusanya ushahidi,” Ingrid Turinawe alisema.
Besigye na wakosoaji wengine wa ndani walipinga
matokeo wakisema yalichakachuliwa, tuhuma ambazo Museveni amezikanusha vikali.
Juzi Jumamosi, tume ya uchaguzi nchini humo
ilitangaza kuwa Museveni alipata asilimia 60.8 ya kura, huku mpinzani wake
mkubwa Kizza Besigye akipata asilimia 35.4.
Waangalizi wa uchaguzi kutoka Ulaya waliukosoa
uchaguzi huo wakisema kuwa tume ya uchaguzi sio huru na kwamba upigaji kura ulitawaliwa
na mazingira ya vitisho.
Chaguzi za mwaka 2006 na 2011 zilitawaliwa na ghasia
kufuatia matokeo, na hivyo kuzusha maandamano nchi nzima, hususan katika mji
mkuu, Kampala.
Museveni, aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya
kuanzisha vita vya msituni, anasifiwa na Waganda wengi kwa kile wanachosema
kuwa ni kazi kubwa ya amani na uthabiti wa kiuchumi aliouleta kiongozi huyo.
0 comments:
Post a Comment