Bwana mmoja mwenye umri wa miaka 65 katika mkoa wa
Aksaray katikati mwa nchi ya Uturuki ameripotiwa kumpa sumu mkewe, akaiba kila
kitu katika nyumba na kukimbia na mwanamke mwenye umri wa miaka 30 ambaye
alikuwa mpangaji wao kwa miezi kadhaa tu.
Kwa mujibu wa ripoti kutoka mji huo, Zeynel D, baba wa
watoto wa nne, ambaye amekuwa kwenye ndoa kwa muda wa miaka 38 alikuwa na
uhusiano wa kimapenzi na mpangaji wake, ambaye naye ni mke wa mtu na ana watoto
wawili.
Mke wa Zeynel D., bibi Cennet D. amedai kuwa wawili hao
walipanga kukimbia, na hivyo wakampa sumu, ili waibe dhahabu yenye thamani ya
lira 100,000 za Kituruki, kilogramu moja ya lulu, yuro 600 na hati za mali
mbalimbali.
Lakini pesa na dhahabu sio vitu pekee walivyoiba na
kukimbia. Imeripotiwa kuwa walichukua kila kitu katika nyumba kuanzia vyombo
vya ndani, kahawa, chai, maziwa na kadhalika.
Mke anasema kuwa mumewe hakuwa na ajira kwa muda wa
miaka 25 hivyo aliinunua nyumba hiyo kwa pesa zake.
"Sikutarajia kitu kama hicho kutoka kwa mwanaume
huyo. Amekuwa mume wangu kwa miaka 38 na tuna watoto 4,” alisema bi Cennet D. na
kuongeza kuwa hali yake sio nzuri na hawezi kutembea, huku akieleza kuwa mumewe
humpigia simu na kutishia kumuua.
Aliendelea kusema kuwa amewasilisha azimio la talaka
pamoja na mashitaka katika jeshi la polisi kwa vitisho anavyopewa na mumewe.
0 comments:
Post a Comment