![]() |
| Picha hii iliyochukuliwa Septemba 30, 2012 ikiwaonesha waandamanaji wanaoipinga serikali wakiwa wamebeba bango lenye picha ya kiongozi wa Washia nchini humo, Nimr Al-Nimr. |
Leo Saudi Arabia imewanyonga watu 47 waliokutwa na hatia
ya “ugaidi”, akiwemo kiongozi mkubwa wa kidini wa madhehebu ya Kishia
anayedaiwa kuchochea maandamano dhidi ya serikali, wizara ya mambo ya ndani
imesema.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 56, Nimr al-Nimr, alikuwa
mhamasishaji wa maandamano yaliyoibuka mwaka 2011 katika eneo la mashariki ya
nchi hiyo yenye Wasunni wengi, ambapo Washia wachache wanalalamika kuwa
wanabaguliwa.
Lakini orodha hiyo haijumuishi mpwa wa Nimr, Ali
al-Nimr, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 alipokamatwa kufuatia maandamano
hayo.
Taarifa hiyo ya wizara, iliyorushwa na shirika la habari
la nchi hiyo (SPA), imesema kuwa watu hao 47 walitiwa hatiani kwa kasumba za
misimamo mikali, kujiunga na makundi ya kigaidi na kutekeleza njama mbalimbali
za kihalifu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Hossein Jaber
Ansari, amesema kuwa Saudi Arabia italipa “gharama kubwa” kwa kumnyonga Nimr
al-Nimr.
"Serikali ya Saudia inakabiliana na wakosoaji wa
ndani kwa kutumia mabavu na mauaji… serikali ya Saudia italipa gharama kubwa
kwa kufuata sera hizo,” alisema Ansari, aliyenukuliwa na shirika la habari la
Iran (IRNA).
Kunyongwa kwa Nimr kunaweza kuchochea ghadhabu ya vijana
wa kishia, kakaye alionya, huku akitaka kuwepo kwa utulivu.
"Hatua hii itawasha hasira za vijana (wa Kishia)”
nchini Saudi Arabia, alisema Mohammed al-Nimr, na kutaka kuwepo kwa vuguvugu la
upinzani wa amani.
"Tunakataa ghasia na makabiliano na serikali,”
alisema.
Aidha, orodha hiyo inajumuisha Wasunni waliotiwa hatiani
kwa kuhusika na mashambulizi ya Al-Qaeda yaliyoua Wasaudia na raia wa kigeni
katika taifa hilo mwaka 2003 na 2004.
Walionyongwa ni pamoja na raia mmoja wa Misri na
mwingine wa India. Wengine wote walikuwa Wasaudia.
Orodha hiyo inamjumuisha Fares al-Shuwail ambaye vyombo
vya habari nchini humo vinamuelezea kuwa kiongozi mkuu wa kidini wa kundi la Al-Qaeda
nchini Saudi Arabia. Alikamatwa Agosti 2004.
Wizara imesema kuwa walinyongwa katika maeneo 12 tofauti
katika miji mbalimbali ya taifa hilo, bila kutoa maelezo ya kina juu ya njia
zilizotumika kuwanyonga.
Kwa kawaida unyongaji nchini humo hufanyika kwa kukata
vichwa vya wahusika kwa kutumia panga.
Adhabu za unyongaji zimeongezeka nchini humo tangu
Mfalme Salman alipokalia kiti cha ufalme Januari 2015 kufuatia kifo cha mfalme Abdullah.
Idadi ya walionyongwa leo ni zaidi ya nusu ya wale
walionyongwa katika kipindi cha mtangulizi wa Salma kwa mwaka wote wa 2014 ambao
ni 87.
Mwaka 2015, Saudi Arabia iliwanyonga watu 153 waliokutwa
na hatia ya makosa mbalimbali, ikiwemo usafirishaji wa madawa ya kulevya.
Mwaka 2011, mamlaka za nchi hiyo ziliweka mahakama
maalumu zinazoshughulikia kesi za raia na wageni wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa
kundi la Al-Qaeda au walioshiriki katika wimbi la mashambulizi yaliyoikumba
nchi hiyo tangu mwaka 2003.
Mashambulizi hayo yaliwaua zaidi ya askari 150 wa nchi
hiyo na raia wengine wa kigeni.
Mwanamfalme wa sasa anayetarajiwa kukalia kiti cha
ufalme, Mohammed bin Nayef, alisimamia
zoezi la kuwashughulikia wanamgambo wakati huo.
Lakini Nimr alikamatwa kwa sababu tofauti mwaka 2012.
Wakati huo wizara ya mambo ya ndani ilimuelezea kama
mchochezi na kutangaza kuwa amekamatwa katika kijiji cha Washia cha Awamiya mashariki
mwa nchi hiyo baada ya kujeruhiwa mguuni wakati akipinga kukamatwa.

0 comments:
Post a Comment