

TAARIFA KUTOKA OFFICE YA WAZIRI MKUU BAADA YA ZIARA YA
KUSHTUKIZA BANDARINI LEO
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amefanya ziara nyingine ya kushtukiza bandarini na kukagua
mfumo wa upokeaji na utoaji mizigo na utozaji wa malipo baada ya kupewa taarifa
kwamba kuna makontena 2,431 yametolewa bila kulipiwa ushuru.
Waziri Mkuu alisema kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa
bandari ya kuanzia Machi hadi Septemba 2014, makontena hayo yalipita bila
kulipiwa kodi kupitia bandari kavu nne (ICDs) ambazo ni JEFAG, DICD, PMM na
AZAM.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni watumishi 10 tu ambao
wamesimamishwa kazi kutokana na makosa hayo. “Mmeamua kuwasimamisha kazi watu
wadogo na kuwaacha wakubwa wanaendelea na kazi. Hatuwezi kuendelea kuikosesha
Serikali mapato namna hii,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amemtaka Kaimu Meneja wa Bandari, Bw. Hebel
Mhanga amletee ofisini majina ya watumishi wote waliohusika na ukwepaji kodi
huo ifikapo leo saa 11 jioni. Pia amempa Meneja huyo wiki moja kuhakikisha kuwa
mamlaka hiyo inabadilisha mfumo wa utozaji malipo kutoka kwenye billing system
na badala yake kuweka mfumo wa malipo wa kielektroniki (e-payment).
Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Desemba 3, 2015),
wakati akikagua idara mbalimbali za mamlaka ya bandari na kuona ukaguzi wa
mizigo unavyofanyika kwa kutumia scanners. Akiwa kwenye chumba cha scanner
mojawapo, Waziri Mkuu alikuta manifest moja ikisema kontena limejaa diapers
lakini picha ya kwenye kompyuta ya scanner ilionyesha kuwa ndani ya kontena
hilo kuna vitu kama vifaa vya umeme.
Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Bandari upande wa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), Bw. Ben Usaje ambaye pia ni msimamizi wa kitengo cha
scanner, inapobainika taarifa kama hiyo inapaswa itumwe kwa wenye ICDs ili
wafanye ukaguzi kwa kulifungua kontena ili kuhakikisha mali zilizomo ndizo
zilizoandikishwa kwenye manifest.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Majaliwa amefanya
ziara ya kushtukiza kwenye ofisi za Shirika la Reli (TRL) na kukagua mabehewa
yaliyokuwepo kisha akazungumza na baadhi ya wafanyakazi waliokuwepo kwenye
stesheni hiyo ambako alibaini madudu kwenye malipo ya mishahara na makato ya
michango ya wafanyakazi.
Akizungumza na Mkurugenzi Mkuu TRL, Mhandisi Elias
Mshana, Waziri Mkuu alisema amefika kwenye shirika hilo ili kujifunza utendaji
wao kazi lakini anazo taarifa za wao kupewa fedha na Serikali kiasi cha sh.
bilioni 13.5/- ili waendeleze miundombinu ya reli lakini hawakufanya hivyo.
“Nia ya kuwapa fedha hizo ilikuwa ni kuboresha miradi ili muweze kujiendesha
kibiashara lakini nyie mkaamua kujilipa wenyewe,” alisema.
“Ninazo taarifa kuwa baada ya hapo, mlikopa sh. bilioni
3 kutoka benki ya TIB ili kuendesha miradi ya shirika lakini badala ya kufanya
miradi, fedha hizo mkaamua nazo kujilipa mishahara. Sasa sijui mnarudishaje huo
mkopo wakati hakuna mradi wowote uliofanyika,” alihoji bila kupata majibu.
Alipoulizwa wafanyakazi wana matatizo gani hapo TRL,
Katibu wa TRAWU, Bw. Boaz Nyakeke alisema wanadai malimbikizo ya makato yao
kwenye mifuko ya pensheni, malimbikizo ya makato kwenye SACCOS na malimbikizo
ya kuanzia Julai – Novemba 2014.
Waziri Mkuu kwa upande wake alimtaka Mhandisi Mshana
asimamie uboreshaji huduma za usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam ili
hata mabasi ya mwendo kasi yatakapoanza wananchi waweze kuwa na uhuru wa
kuchagua aina ya usafiri wautakao.
“Tunataka kujenga yadi kubwa nje ya mji ili watu wenye
magari wawe wanayaacha huko na kutumia usafiri wa treni au DART kuja mjini kama
njia mojawapo ya kupunguza msongamano wa magari jijini Dar es Salaam,” alisema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021, 11410 DAR ES SALAAM
ALHAMISI, DESEMBA 3, 2015.
0 comments:
Post a Comment