Dear Uncle Magufuli,
Japo salamu hii hufaa kutamkwa kwa mdomo, lakini acha tu
niseme Shikamoo Uncle Magu. Pole na kazi. Mimi sijambo kabisa. Nilitaka
kukupigia simu lakini haina chaji nimeipeleka kwenye duka la Mtifuamchwa
kuchaji, si unajua ndiye mtu pekee mwenye jenereta hapa kijijini kwetu!

Uncle najua unaielewa vyema hali yangu lakini kama
unijuavyo mimi huwa sipendi kukuomba chochote labda kama ukiamua kunitumia.
Kusema na ule ukweli maisha ni magumu sana. Jana nilikula mlo mmoja tu na leo
sina uhakika wa kupata chochote cha kuweka tumboni. Nilikuwa na Malaria juzi
nimekunywa tu mwarobaini sababu sina hela ya kununua dawa.
Tuachane na hayo, kiukweli Uncle pamoja na hivyo roho
yangu bado inasita kukupigia simu kwa kitendo nilichokifanya. Sijui kama
utanielewa. Naona aibu sana kwa kutokukuamini. Najutia kutokukuamini. Najuta
kutokupa kura yangu.
Sikatai, ulikuwa na maneno ya kushawishi sana kwenye
kampeni zako lakini nilikumbuka kuwa hayo yamewahi kusemwa sana na
waliotangulia lakini bado maisha yetu yameendelea kuwa magumu. Maisha yetu ni
magumu sana Uncle.
Nilijidanganya kuwa ningekupa kura yangu ningekuwa
namleta mtu atakayeendelea na uongozi wa kubebana, uongozi wa business as
usual, unaoruhusu watu wachache kufanya watakalo na kula robo tatu ya keki ya
taifa. Najilaumu kukariri. Najilaumu kutilia shaka ahadi zako. Kama uchaguzi
ungefanyika leo nisingejifikiria mara mbili kukupigia kura.
Kiukweli, wewe mwenyewe unajua jinsi ambavyo chama chako
kilikuwa kimepoteza uaminifu kwa wananchi. Naamini si mimi tu ninayejuta
kupitiwa na upepo huo wa kutokiamini chama chako na kudhani ni kosa kubwa
kukupa nafasi wewe kwakuwa ulikiwakilisha. Uncle Magu, tangu uingie madarakani,
sikosi kuangalia taarifa ya habari kwenye TV kwa Mtifuamchwa kuangalia ni kitu
gani kipya umekifanya. Unanipa raha sana.
Yaani una siku 27 tu tangu uingie madarakani lakini
umefanya mambo makubwa kuliko kawaida. Nasikia umepata umaarufu mkubwa barani
Afrika. Nilisoma gazeti moja wameandika kuwa sijui kuna mtandao wa kijamii
unaitwa Twira kwamba Afrika nzima ilikuwa ikikujadili kwa kasi yako. Nasikia
nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Malawi, Zambia na hata Australia
wanatamani wangekuwa na kiongozi kama wewe. Yaani naskia raha sana kila nisikiapo
jina lako likitajwa.
Nasikia siku hizi maofisini wafanyakazi wanawahi
utadhani enzi zile nilivyokuwa nikiwahi namba asubuhi ili kuepuka viboko vya
mwalimu wa zamu! Huku kwetu utafanya surprise lini? Kuna manesi kwenye kile
kituo chetu cha afya wanachambua mchele kazini na kuwaacha wagonjwa
wakihangaika tu! Njoo uwanyooshe na huku.
Kweli nimeamini kuwa mtu mmoja anaweza kubadili kabisa
mwelekeo wa nchi. Unapataje ujasiri huo Uncle? Umenifurahisha sana ulivyofuta
safari za nje. Nasikia umeokoa mabilioni ya fedha kutokana na safari hizo.
Yaani kweli Uncle hawa viongozi waanze kuja na huku vijijini wajionee maisha
tuliyonayo, tunaishi kwa tabu. Pale Muhimbili ulichokifanya unastahili sifa
kwakweli.
Unafanya kazi nzuri hadi wananchi wa nchi jirani
wanatamani ungekuwa rais wao. Nasikia wanataka wakukodi ili ukawanyooshe pia.
Hata hivyo haiwezekani. Lakini viongozi wao watajifunza mambo mengi kutoka
kwenye uongozi wako.
Halafu Uncle huyu Kassim Majaliwa siku umemtangaza kuwa
waziri mkuu nilipata wasiwasi kama angeiweza kasi yako. Lakini naye ni jembe
aisee. Ulimjuaje? Yaani mnachokifanya ni sawa na ile movie ya The Expendables!
Wewe ni Sylvester Stallone, Majaliwa ni Wesley Snipes na Ombeni Sefue ni Dolph
Lundgren, yaani ni kichapo kwa kwenda mbele!
Alichokifanya Majaliwa pale bandarini kimevumbua madudu
mengi. Hivi hawa watu wa TRA wanataka kuifilisi nchi? Kumbe ndio maana watoto
wao wanasoma shule za nje na kuishi kwenye majumba ya kifahari. Hivi hizo hela
za kodi zingepatikana si zingesaidia kutujengea hii zahanati yetu hapa kwetu.
Uncle hivi unaamini kuwa hadi leo tunaenda kutibiwa kwenye kile kituo cha afya
kilicho karibu na mashamba ya bibi? Kule kuna umbali wa kilomita 13.
Uncle baraza lako la mawaziri utalitaja lini? Nasikia
wabunge wengi wanaogopa kasi yako. Wengi walizoea kula bata na kupishana
airport utadhani nchi yetu ina vita. Watauweza muziki wako wa Hapa Kazi tu?
Nina hamu ya kulisikia baraza lako, fanya ulitangaze sasa Uncle.
Uncle mimi nina imani sana na wewe kuwa utainyoosha hii
nchi. Umeichukua ikiwa katika hali mbaya sana. Umeikuta katika hali ambayo kuna
baadhi ya watu wanaishi kama miungu watu. Kwa fedha za serikali watu wamegeuka
kuwa mabilionea. Ona kama wale waliokula shilingi trilioni 1.3 za Stanbic! Hivi
hawa watu hizi hela zote wanazipeleka wapi? Fedha hizi zingepelekwa vyuoni
wanafunzi wote wangepata mikopo kwa asilimia mia. Uncle unajua kuwa ni shilingi
bilioni 345 tu zilitengwa katika mwaka wa fedha uliopita (2014/2015) kwaajili
ya mikopo ya wanafunzi 98,000? Sasa hebu jiulize wanafunzi wangapi wangepata
mikopo!
Kama fedha zinazoliwa na mafisadi wachache
zikikombolewa, naaamini walimu, polisi, wauguzi na wafanyakazi wengine wa chini
wa serikali watakuwa na mishahara mizuri. Sina shaka na wewe naamini mpaka
mwishoni mwa mwaka 2016 heshima itakuwa imerudi mjini.
Uncle mimi ninaamini kuwa hadi June mwaka huu ugonjwa
utakaosumbua maofisa wengi wa juu utakuwa ni pressure. Wakimbize hivyo hivyo
atakayeshindwa kasi yako na kukubali maisha ya kupata kipato halali apishe
wengine.
Uncle Magu, walinzi wako wamejipanga vizuri
kukuhakikisha usalama wako? Nina wasiwasi katika safari yako utatengeneza
maadui wengi na wengine ambao wana nguvu kubwa kifedha. Najua kasi yako
itawakosesha ulaji mapapa wengi na hawatakuwa na furaha na wewe kwahiyo naomba
uimarishe kidogo ulinzi wako.
Wananchi wa kawaida wanakuombea sana ufanye kazi yako
bila kuchoka. Tunakuombea uwe na busara zaidi ili wale wanakuombea uteleze
katika maamuzi yako wabaki na aibu zao. Endelea kuwashangaza kila kukicha.
Uncle nisikuchoshe kwa barua ndefu. Naamini umenisamehe
kwa kukusaliti. Naomba tu ukipata nafasi unikumbuke hata kaelfu 20 katanisaidia
kidogo. Mungu akubariki Uncle Magu.
Ndimi mpwa wako, Shidondofilo.
Imeandikwa na Fredrick ‘Skywalker’ Bundala.
0 comments:
Post a Comment