
RAIS wa Uturuki Recep
Tayyip Erdoğan mapema leo amesema kuwa nchi hiyo ina ushahidi kwamba Urusi
inajihusika na biashara haramu ya mafuta kutoka kundi la Dola ya Kiislamu nchini Syria (ISIS), hali inayoonekana kama
majibu dhidi ya tuhuma za Urusi kwamba Uturuki inanunua mafuta kutoka kundi
hilo.
Jana Jumatano wizara ya ulinzi ya Urusi ilimtuhumu Erdoğan
na familia yake kuhusika na biashara hiyo baada ya Ankara kutungua ndege ya
kivita ya Moscow mwezi uliopita jambo lililouzamisha uhusiano wa nchi hizo
katika mgogoro.
"Katika siku za hivi karibuni umeibuka mtindo
unaoongozwa na Urusi. Hakika, hata Urusi haiamini hili pia,” alisema Erdoğan, akikusudia
tuhuma za kuhusika na baishara ya mafuta kutoka kwa kundi hilo.
"Tazama, Urusi inatakiwa kuthibitisha kuwa Jamhuri
ya Uturuki inanunua mafuta kutoka kwa kundi la Daesh, vinginevyo haya ni
masingizio,” alisema, huku akisisitiza kuwa atajiuzulu iwapo Urusi itaweza
kuthibitisha madai hayo.
"Nani anayenunua mafuta kutoka kwa Daesh? Ngoja niseme.
George Haswani, mwenye pasipoti ya Urusi na uraia wa Syria, ni miongoni mwa
wafanyabiashara wakubwa wa shughuli hizi,” alisema Erdoğan.
Mwezi Novemba, Wizara ya Fedha ya Marekani ilimuwekea
vikwazo Haswani, ambaye pia aliwekwa kwenye orodha ya vikwazo ya Muungano wa
Ulaya, kwa kufanya kazi kama mtu wa kati kwa ajili ya ununuzi wa mafuta
unaofanywa na serikali ya Syria kutoka kundi hilo la Daesh (ISIS).
Erdoğan amesema “mchezaji maarufu wa santaranji kutoka
Urusi” anahusika pia na biashara hiyo ya mafuta, bila kumtaja jina. “Naye yumo
katika mashindano haya,” alisema.
Aidha, vikwazo vya Marekani vilimkumba Kirsan
Ilyumzhinov, tajiri wa Kirusi na rais wa muda mrefu wa Shirikisho la Mchezo wa
Santranji Duniani (FIDE) ambaye aliwahi kuwa mkuu wa jimbo la Kalmykia kusini
mwa Urusi.
Jumatano Marekani ilikanusha madai ya Urusi kwamba
Uturuki inahusika na ununuaji wa mafuta ya Daesh.
Josh Earnest, msaidizi wa rais na msemaji katika Ikulu
ya ametupilia mbali madai hayo na kumlaumu Assad kuwa anahusika na biashara ya
mafuta kutoka kundi hilo.
0 comments:
Post a Comment