![]() |
| Wasichana wapatao 170 waliotoroka kukimbia ukeketaji katika eneo la Magumu katika Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, wakiwa wamekusanyika katika kituo cha Nyumba Salama walikopewa hifadhi kabla ya kuunganishwa na familia zao na kuanza masomo. |
Jumla ya wasichana 2,118 wametoroka maskani yao tangu
Novemba 15 mwaka huu kukwepa vitendo vya ukeketaji katika maeneo kadhaa ya mkoa
wa Mara.
Wasichana hao wamepewa hifadhi katika Kituo cha Uokozi
cha Masanga kinachoongozwa na Kanisa Katoliki wilayani Tarime. Baadhi ya
wasichana hao wamesema kuwa wanakutana na changamoto ya kukubaliwa na familia
zao kwa sababu ya kukimbia vitendo hivyo vya kimila.
Catherine Johannes na Angel Charles walisema kuwa ni
wakati sasa kwa jamii kusimama na kuungana pamoja kupinga vitendo hivyo.
“Tunatoa wito kwa serikali na kwa kila mwanajamii
kukomesha vitendo hivi. Wasichana wengi hawavifurahii kwa sababu
vinatudhalilisha na kuathiri mipango yetu ya baadae,” anasema Catherine.
Katibu wa kituo hicho, Dickson Joseph, aliitaka serikali
kuimarisha sheria ili adhabu kali, ikiwemo kifungo cha maisha, itolewe dhidi ya
wale wanakandamiza na kudhulumu haki za wasichana.
“Tunahitaji sheria imara na kali ili kukomesha vitendo
hivyo vya kikatili,” alisema.
Mamlaka za serikali mkoani Mara na wanaharakati dhidi ya
ukiukaji wa haki za wanawake wanatarajia kuanzisha vituo vya uokozi ili
kuwaokoa wasichana dhidi ya ukeketaji.
Ukeketaji ni kinyume cha sheria lakini baadhi ya jamii
zimeendelea kushikilia utamaduni huo, ambao huwasababishia wasichana
udhalilishaji na maumivu makali. Inakadiriwa kuwa mwaka jana, zaidi ya
wasichana 1,600 walikeketwa katika vijiji kadhaa vya Wilaya ya Tarime pekee.

0 comments:
Post a Comment