
Uingereza imeripotiwa kuanza mashambulizi yake dhidi ya
maeneo ya kundi la Dola la Kiislamu nchini Syria baada ya serikali kupata
idhini ya bunge ya kufanya mashambulizi hayo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, duru za
serikali zimesema kuwa Uingereza imeanza mashambulizi yake ya ndege nchini
Syria.
Serikali hiyo haijaweza wazi undani wa mashambulizi
hayo, lakini ripoti za vyombo vya habari zimemnukuu Waziri wa Ulinzi wa
Uingereza Michael Fallon akisema kuwa ndege zake zimeshambulia visima vya
mafuta mashariki mwa Syria.
Hatua hiyo imefuatia mjadala mkali uliodumu kwa saa 10
mapema Jumatano, ambapo wabunge 397 walipiga kura kuiunga mkono huku wengine
223 wakipinga hatua ya Uingereza kupanua mashambulizi yake ya ndege kutoka Iraq
mpaka Syria.
Kufuatia kura hiyo, Waziri Mkuu wa Uingereza aliusifu
uamuzi huo kwa kuuita kuwa ni “uamuzi sahihi” akisema, “ninaamini bunge limechukua
uamuzi sahihi wa kuendelea kuifanya Uingereza kuwa salama… hatua ya kijeshi
nchini Syria ni sehemu ya mkakati wetu mpana.”
Cameron alikuwa miongoni mwa waungaji mkono wakubwa wa
upanuzi wa mashambulizi ya anga ambayo ni sehemu ya ushirika unaoongozwa na
Marekani dhidi ya maeneo yanayoshikiliwa na kundi hilo nchini Iraq.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uingereza, Philip
Hammond, aliikaribisha taarifa hiyo akisema kuwa Uingereza imekuwa “salama
zaidi kwa sababu ya hatua iliyochukuliwa na wabunge”. Mashambulizi ya kijeshi
pekee hataisaidia Syria, hatatufanya tuwe salama dhidi ya Daesh lakini. Lakini msimamo
huu wa pamoja utatusaidia.”
Muda mfupi baada ya kura hiyo ya bunge, ndege za
Uingereza ziliruka kutoka kambi ya jeshi la anga ya Akrotiri nchini Cyprus. Mahali
zilikoelekea hapajulikani na watawala wa Uingereza hawakuwa tayari
kulizungumzia.
Wakati wa mjadala bungeni, Cameron aliwataka wabunge
kuitikia wito wa washirika wao na kuchukua hatua dhidi ya kundi la Dola la
Kiislamu ambalo linataka kuwaua na kuwapachika kasumba watoto wao.
"Je, tushirikiane na washirika wetu kukabili
kitisho hiki na kuwafuata magaidi hawa katika maeneo yao wanayopanga kuwaua
Waingereza, au tukae na kutusubiri watushambulie?” alisema.
Kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn, alipinga
hatua hiyo lakini akawapa uhuru wabunge wa chama chake kuiunga mkono au
kuikataa.
Katika kujibu hotuba ya Cameron, Corbyn alisema, “Haiwezekani
kuepuka hitimisho kuwa waziri mkuu anatambua upinzani wa umma dhidi ya wazo
lake bovu la kukimbilia kwenye vita… na anataka kura ifanyike kabla mambo
hayajamwendea kombo. Ni wazi kuwa mawazo ya waziri mkuu ya kuchukua hatua za
kijeshi hayakubaliki”.
Katika andiko lake kwenye mtandao wa Facebook alililolichapisha
baada ya kura ya bunge, Corbyn alirejea msisitizo wa kuutafutia mgogoro huo
suluhisho la amani, akasema: “Nimekuwa nikisisitiza na nitaendelea kufanya
hivyo kwamba, tunatakiwa kuongeza mara dufu juhudi za kutumia njia za
kidplomasia na kisiasa kumaliza mzozo wa Syria.”
“Askari wa Uingereza watakuwa hatarini na upotevu wa
maisha ya watu wasiokuwa na hatia hautakwepeka,” aliandika Corbyn.
Rais wa Marekani Barack Obama aliukaribisha uamuzi huo
na kusema: “Tangu tulipoanza mapambano dhidi ya ISIL, Uingereza imekuwa
miongoni mwa washirika wetu wa thamani kabisa katika mapambano hayo. Tunatarajia
kuona vikosi vya Uingereza vikiungana na vikosi vya washirika katika anga ya
Syria, na tutawajumuisha katika vikosi vya anga vya ushirika wetu haraka
iwezekanavyo.”
Aidha, Obama aliusifu uamuzi wa hivi karibuni wa
serikali ya Ujerumani kutuma askari 1,200 kushiriki mapambano dhidi ya ugaidi
nchini Syria.
Tangu Agosti 2014, Marekani na baadhi ya washirika wake
wamekuwa wakifanya mashambulizi ya anga dhidi ya maeneo yanayokaliwa na kundi la
Dola la Kiislamu nchini Iraq.
Baadhi ya washirika hao wamekuwa wakifanya hivyo nchini
Syria bila idhini ya Damascus au Umoja wa Mataifa tangu Septemba mwaka jana.
0 comments:
Post a Comment