![]() |
| Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa, Jaji Mstaafu Damian Lubuva |
WATU wawili wakiwemo Mwanasheria na Mwalimu,
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam
wakikabiliwa na mashitaka ya kula njama za kumuua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa
ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva na familia yake.
Washitakiwa hao, Mwalimu Samwel Gikaro (30) na
Mwanasheria Angela Mbonde (32) walifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa
mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi Thomas Simba.
Wakili wa Serikali, Hellen Moshi alidai kati ya Oktoba
23 na Novemba 16, mwaka huu katika maeneo tofauti Dar es Salaam na maeneo
mengine nchini, washitakiwa na wengine ambao hawajafika mahakamani, walikula
njama za kumuua Jaji Lubuva na familia yake.
Washitakiwa walikana mashitaka na upande wa Jamhuri
ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya
kutajwa. Wakili wa upande wa utetezi, Moses Kaluwa ambaye alifika mahakamani
hapo kwa niaba ya Wakili Peter Kibatala, aliiomba mahakama itoe dhamana kwa
washitakiwa kwa kuwa mashitaka yanayowakabili yana dhamana.
Wakili Moshi alidai Jamhuri inatambua mashitaka hayo
yana dhamana kisheria, lakini inaomba dhamana izuiliwe kwa muda hadi
watakapoona inafaa kwa sababu ya asili ya kosa, washitakiwa hawawezi kuwa nje
wakati upelelezi unaendelea.
Hata hivyo, Wakili Kaluwa alidai sababu zilizotolewa na
upande wa jamhuri hazina msingi kisheria, suala la msingi ni mashitaka
yanayowakabili kuwa na dhamana na washitakiwa wapo tayari kutimiza masharti
yatakayotolewa na mahakama.
Hakimu Simba alisema pamoja na mashitaka hayo kuwa na
dhamana kisheria, kutokana na kosa pamoja na hatua ya upelelezi, mahakama
imekubali hoja za upande wa jamhuri hivyo washitakiwa watakuwa rumande. Kesi
itatajwa tena Desemba 15, mwaka huu.
CHANZO: Habari Leo

0 comments:
Post a Comment