Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa masharti matano
kwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), yanayotakiwa kutekelezwa kabla
kupewa msamaha wa kodi kwa gari aina ya Iveco ulioombwa.
Hatua hiyo imekuja baada ya Bakwata kuiomba TRA msamaha
wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa barua yenye kumbukumbu
MK.TRAIJAV.51707 iliyoandikwa Oktoba 9, mwaka huu.
Akijibu maombi hayo kwa barua ya Novemba 19, 2015,
Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, Mwantum Salimu alisema takwimu za mamlaka
hiyo zinaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la misamaha ya kodi kwa
Bakwata.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Bakwata, Sheikh Suleiman
Lolila alisema wamepokea barua hiyo ya TRA na wanaifanyia kazi kwa sababu mambo
yanayohitajika ni ya muda mrefu, hivyo wakikamilisha wataijibu.
Salimu alisema tangu mwaka 2006 hadi Septemba 2015 kuna
magari ya Bakwata 82 ya aina tofauti yaliyopewa msamaha.
Alisema kutokana na idadi kubwa ya magari
yaliyokwishasamehewa kodi, kabla ya kuendelea na mchakato wa maombi hayo,
Bakwata wanatakiwa kuwasilisha taarifa mbalimbali TRA.
Mwamtumu alisema katika kipindi cha siku saba, Bakwata
wanatakiwa kuwasilisha kadi za usajili wa magari yaliyosamehewa kodi.
Alisema pia wanatakiwa kuwasilisha kitabu kinachoonyesha
safari za magari na majina ya madereva wa magari.
Ofisa huyo wa TRA aliagiza baraza hilo kuwasilisha
risiti za kulipia mafuta, bima na matengenezo ya magari hayo.
“Mnatakiwa kuleta maelezo ya ushahidi kuhusu fedha
zilizotumika kununua magari hayo pamoja na hesabu za mwaka za taasisi
zilizokaguliwa,” alisema ofisa huyo katika barua yake.
Alisema ili kushughulikia msamaha wa kodi wa gari hilo
lenye namba ya chasis WJME2NM- 4000428502, baraza inatakiwa kuwasilisha
mahitaji hayo katika muda uliopangwa.
“Ili mamlaka iweze kushughulikia maombi yenu ya msamaha
wa kodi tunaomba mlete mahitaji kama tulivyoelekeza,” alisema katika barua
ambayo Mwananchi imeona nakala yake.
Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipakodi wa
TRA, Richard Kayombo alikiri mamlaka hiyo kuandika barua hiyo huku akishangaa
namna barua hiyo ilivyofika mitandaoni.
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment