|  | 
| Melissa Fleming, msemaji wa UNHC. | 
Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia wakimbizi
(UNHCR) limeonya kuwa maneno makali katika kampeni nchini Marekani dhidi ya
wakimbizi na Waislamu yanaathiri programu ya nchi hiyo ya makazi kwa ajili ya
Wasyria na wakimbizi wengine.
Mtia nia wa kiti cha urais wa chama cha Republican, Donald
Trump, jana alitoa wito wa “kuwazuia kabisa” Waislamu kuingia nchini Marekani
katika jibu lake dhidi ya mashambulizi yaliyotokea wiki iliyopita katika mji wa
San Bernardino, California, ambayo yalisababisha vifo vya watu 14 na kuwajeruhi
wengine 21.
Msemaji wa UNHCR, Melissa Fleming, akiongea na vyombo
vya habari mjini Geneva amesema kuwa “(Trump) alizungumzia watu wote lakini pia
hili linaathiri programu ya wakimbizi.”
“Kwa sababu programu yetu ya wakimbizi haibagui dini,”
alisisitiza. “Programu yetu ya makazi inawachagua watu ambazo wana uhitaji
mkubwa.”
Marekani imewapa hifadhi wakimbizi wapatao 1,500 pekee
kutoka Syria tangu mwaka 2011.
Utawala wa Obama unapanga kuwapokea wakimbizi 10,000 kutoka
Syria mwaka huu. 
Fleming alielezea wasiwasi wake kuwa magavana wa
Marekani wapatao 40 wanapinga mpango huo.
"Tuna wasiwasi kuwa maneno yanayotumika katika
kampeni za uchaguzi zinauweka hatarini mpango huu muhumi ambazo unakusudia
kuwasaidia watu wenye shida na ambao ni waathirika wa vita ambavyo dunia
imeshindwa kuvikomesha," alisema.
Shirika hilo linaitaka Marekani kuwapokea wakimbizi 75,000
kutoka Mashariki ya Kati, Afrika na kwingineko mwaka huu.
|  | 
| Mgombea urais wa chama cha Republican, Donald Trump. | 
Huko nyuma Trump aliwahi kusema kuwa angewafukuza
wakimbizi wote wa Syria kama atachaguliwa kuingia Ikulu ya Marekani.
Kampeni za Trump zimekuwa zikigubikwa na maelezo yenye
utata dhidi ya wahamiaji, wakimbizi na Waislamu.
 
0 comments:
Post a Comment