WATOTO wawili wenye umri wa miaka minne na mitano,
wakazi wa wilaya ya Ukerewe, Mwanza wanauguza majeraha ya mikono yao baada ya
shangazi yao kuwachoma moto akiwatuhumu kuiba kitoweo.
Asha Ramadhani (4) na Ismaili Ramadhani (5) walikumbwa
na mateso hayo Desemba 21 usiku wakiwa nyumbani kwa shangazi yao katika
kitongoji cha Stooni, kata ya Nakatungulu, mjini Nansio.
Mkuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) ya Ukerewe, Ally Mkalipa
amethibitisha kuwapo tukio hilo ambalo mtuhumiwa ni Ashura Ismail (30) na
kuongeza kuwa, uchunguzi umekamilika na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati
wowote.
“Ni kweli tumepokea malalamiko hayo na baada ya kumhoji
mtuhumiwa amekiri kutenda kosa kwa kile alichodai kupatwa na hasira baada ya
watoto hao kukaidi mara kwa mara maelekezo yake,” alisema Mkalipa.
Shangazi wa watoto hao, akijitetea, alidai watoto hao
waliokuwa wakiishi na baba yao katika kambi za uvuvi, ni watukutu na kwamba
wakionywa hawatii. Alidai, kwa muda mrefu kaka yake ambaye ni baba wa watoto
hao aliwatelekeza nyumbani kwake bila ya kutoa msaada wa aina yoyote.
Aliendelea kujitetea kwamba, kitendo cha kubeba mzigo
mkubwa pia ndilo tatizo linalochochea hasira na kusababisha achukue hatua hiyo.
Kwa upande wao watoto, walidai mbali ya kupewa adhabu hiyo ya kuchomwa moto
viganja vya mikono, pia walikuwa wakipigwa mara kwa mara na kunyimwa chakula.
Walisema wamekuwa wakipata msaada wa chakula kutoka kwa
majirani. Mmoja wa wakazi wa kitongoji cha Stooni, Mazoto Chrisant
alithibitisha kwamba watoto hao wamekuwa wakila nyumbani kwake mara kwa mara.
Chrisant alisema siku watoto hao walipochomwa moto,
alishindwa kuvumilia kitendo hicho ndipo akaamua kufikisha suala hilo kwa
watetezi wa haki za binadamu. Mtetezi wa Haki za Binadamu, Daniel Kondayo
anayeishi na watoto hao kwa sasa, alisema wanaendelea kupata tiba na chakula
chenye lishe kutokana na miili yao kudhoofu.
Ilielezwa kwamba, baada ya watoto hao kupelekwa
hospitali, uchunguzi wa kitabibu ulibaini licha ya majeraha ya moto waliyo
nayo, wanakabiliwa na magonjwa ya homa ya tumbo, malaria na utapiamlo.
CHANZO: Habari Leo

0 comments:
Post a Comment