TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Na Ibrahimu Lipumba.
30 Disemba 2015
MSAADA WA MAREKANI NA UCHAGUZI WA ZANZIBAR
Moja ya mafanikio makubwa ya Rais Kikwete ni kuimarisha
uhusiano wa Tanzania na mataifa makubwa hususan Marekani na China. Rais Kikwete
alifanikisha Tanzania kupata msaada mkubwa wa Millennium Challenge Corporation
– MCC wa dola milioni 698 kutoka serikali ya Marekani uliogharamia miradi mingi
ya sekta ya usafiri, nishati na maji katika kipindi cha miaka 5 kati ya 2008 –
2013.
Naunga mkono azma ya Rais Magufuli ya kupunguza na
hatimaye kuondoa kabisa nchi yetu kuwa tegemezi wa misaada ya nje. Pamoja na
lengo hilo ni muhimu kuyalinda na kuyatumia kwa manufaa ya taifa matunda ya
diplomasia ya JK.
Serikali ya awamu ya nne ilifanikisha maandalizi ya
kupata msaada wa pili wa dola milioni 472.8 ambao utajikita katika kuimarisha
sekta ya nishati ili kuhakikisha kupatikana kwa umeme wa uhakika. Uamuzi wa
kuweka kipaumbele sekta ya nishati ulitokana na utafiti wa vikwazo vya uchumi
uliobainisha kuwa ukosefu wa umeme wa uhakika ni kikwazo kikubwa kinachozuia
ukuaji wa uchumi.
Msaada huu wa pili unaojumuisha dola milioni 58.6 zitakazotumiwa
kuimarizha ZECO na sekta ya umeme Zanzibar uko hatarini kusambaratika ikiwa
maamuzi ya wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 2015
hayataheshimiwa.
Serikali imeandaa mpango kabambe wa kurekebisha sekta ya
umeme – Electricity Supply Industry Reform Strategy and Roadmap. Mpango wa pili
wa MCC umejielekeza kusaidia kutekeleza mpango huu wa serikali. Utekelezaji wa
mpango huu pia unalenga kuunganisha wateja wapya 300,000 wapate umeme wa
uhakika. Msaada huu pia unatarajia kurekebisha sekta ya umeme ya Zanzibar na
kuanzisha ufuaji wa umeme wa MW 5 kutumia jua au upepo.
Tarehe 17 Septemba 2015, Bodi ya MCC ilikutana katika
kikao chake cha kila robo mwaka na ikatoa taarifa ya mjadala wake wa msaada wa
pili kwa Tanzania wa dola milioni 472.8. Bodi iliunga mkono msaada huo kwani
una lengo la kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika Tanzania. Msaada huu
utaimarisha utendaji wa asasi zinazosimamia ufuaji na ugawaji wa umeme –
TANESCO kwa upande wa Tanzania Bara na ZECO kwa upande wa Zanzibar.
Hata hivyo Bodi ya MCC ilikuwa na wasiwasi kuhusu rushwa
na ufisadi nchini Tanzania. Ilisisitiza kwamba Tanzania lazima ifaulu kigezo
cha kupambana na rushwa kabla ya kuamua kupitisha msaada huo. Bodi pia ilieleza
kuwa ina matumaini ya uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa tarehe 25 Oktoba 2015
utakuwa huru na haki kwa kuwa MCC inaamini haki za kidemokrasia ni sehemu
muhimu ya utawala bora.
Tarehe 26 Septemba MCC ilitoa tamko kuwa kufuatana na
taarifa za kigezo cha kupambana na rushwa kinachotolewa na Benki ya Dunia
katika chapisho lao la Worldwide Governance Indicators, Tanzania imefaulu
kigezo hiki. Kwa hiyo Tanzania imefaulu vigezo vyote vya kitakwimu
vinavyotumiwa na Bodi katika maamuzi yake. Tamko la MCC liliendelea kusisitiza
matumaini yake kuwa uchaguzi wa tarehe 15 Oktoba 2015 utakuwa huru na wa haki.
Pamoja na mapungufu ya uchaguzi mkuu, Watazamaji wengi
wa ndani na nje waliutathmini mchakato mzima wa uchaguzi kwa ujumla wake na
kuridhishwa kwamba ulikuwa huru na wa haki, Tanzania Bara na Zanzibar.
Watazamaji hawa walistushwa na kustajabishwa na uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kufuta uchaguzi wote wa Zanzibar. Ikumbukwe Zanzibar
wamefanya uchaguzi wa Rais wa Muungano, Wabunge, Rais wa Zanzibar, Wawakilishi
na Madiwani. Uchaguzi huu umetumia Daftari la Wapigakura la ZEC na vituo vya
kupigia kura vilivyoandaliwa na ZEC. Itakuwaje matokeo ya uchaguzi wa Rais wa
Muungano na Wabunge ukubaliwe, lakini Uchaguzi wa Zanzibar ufutwe?
Tarehe 16 Disemba, Bodi ya MCC ilikutana na ikamua
kutopitisha msaada wa pili kwa Tanzania. Hoja kubwa iliyoifanya Bodi isipitishe
msaada wa dola milioni 472.8 ni kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar
baada ya kufanyika uchaguzi mzuri na wa amani. Hoja ya pili ni matumizi mabaya
ya sheria ya Makosa ya Jinai ya Mtandao wakati wa uchaguzi mkuu ambapo kuna
baadhi ya watazamaji waliosajiliwa na Tume ya Uchaguzi walikamatwa na polisi
kwa kutumia sheria hii.
Ni wazi kabisa kama matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar
hayataheshimiwa, msaada wa pili wa MCC utafutwa.
Ikiwa msaada wa pili wa MCC utafutwa utaathiri
utekelezaji wa mpango wa serikali wa kurekebisha sekta ya umeme na pia kuhujumu
mpango wa Rais Obama wa Power Africa kwa upande wa Tanzania. Ziara ya Rais
Obama nchini Tanzania iliambatana na uzinduzi wa Power Africa mpango wa
Marekani kusaidia nchi za kiafrika kuongeza uzalishaji na usambazaji wa umeme.
Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi 6 za mwanzo kufaidika na mpango huu.
Marekebisho ya sekta ya umeme yatakayofadhiliwa na MCC yalitarajiwa kuwa
motisha kwa wawekezaji wa sekta binafsi. Kwa mfano kampuni ya Symbion ambayo
ilitekeleza baadhi ya miradi ya msaada wa kwanza wa MCC, ina mpango wa kuwekeza
ufuaji wa umeme wa MW 600, mjini Mtwara na kuunganisha Mtwara na gridi ya taifa
kupitia Songea. Mradi huu utagharimu zaidi ya dola bilioni 1. Ikiwa msaada wa
MCC utafutwa mradi huu utakuwa mashakani kutekelezwa.
Ilani ya uchaguzi ya CCM inalenga kuongeza uwezo wa
kufua umeme kwa karibu mara tatu, kutoka MW 1308 za sasa mpaka kufikia MW 4915
mwaka 2020. Kuunganisha mikoa yote kwenye gridi ya taifa na kuhakikisha
asilimia 60 za kaya zote zinatumia umeme. Haya ni malengo makubwa sana
yaliyojikita katika utekelezaji wa Mpango Kabambe wa serikali wa sekta ya umeme
utakaosaidiwa na msaada wa MCC.
Kutoyakubali matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar kutaathiri
mahusiano yetu na nchi nyingine hasa za Jumuiya ya Ulaya. Hata Jamhuri ya Watu
wa China inataka nchi yetu iwe na amani na utulivu wa kisiasa. Suala la
Zanzibar la kuheshimu matokeo ya uchaguzi siyo la kusalimu amri ya Mataifa mengine
bali la kuheshimu uamuzi wa Wazanzibari waliofanya kwenye uchaguzi ambao kwa
ujumla wake ulihesabiwa kuwa ni huru na wa haki
Dr Ali Mohamed Shein, Rais aliyechaguliwa katika
uchaguzi wa 2010 ana ufunguo wa tatizo hili. Akubali matokeo ya uchaguzi wa
2015 ya Zanzibar yakamilishwe na kutangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar.
Ajiulize suala la msingi anataka kuleta vurugu za kisiasa Zanzibar? Anataka
kuwapa fursa watu wenye siasa kali inayopinga demokrasia kuhamasisha vijana wa
Zanzibar? Anataka kuharibu matunda ya diplomasia ya JK aliyoshiriki kuyaleta
kama Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaania? Anataka kuvuruga
uhusiano wa Tanzania na Marekani na mataifa mengine? Anataka kumuhujumu Rais
Obama asifanikishe Mpango wake wa Power Afrika kabla hajan’gatuka mwaka 2016?
Anataka kumuharibia Rais Magufuli asitekeleze sera zake za kupambana na rushwa
na kujenga uchumi wa viwanda unaoongeza ajira na kutokomeza umasikini bali
ashughulikie matatizo ya kisiasa na kiusalama ya Zanzibar na kushutumiwa kuwa
anavunja haki za binadamu za Wazanzibari? Anataka Watanzania wa Bara tufanye
maandamano ya kumshutumu kuwa anatuvurugia nchi na kuhujumu utekelezaji wa sera
za Rais Magufuli?
Pamoja na mapungufu yetu, Tanzania inatazamwa kuwa nchi
ya mfano kwa amani na utulivu na ujenzi wa demokrasia katika eneo letu la
Afrika ya Mashariki na nchi za Maziwa Makuu. Tunategemewa kusaidia kusuluhisha
migogoro ya nchi za jirani. Rais Magufuli na Waziri wa Mambo ya Nje, Dr Mahiga
watawezaje kusuluhisha migogoro ya nchi za jirani ikiwa Zanzibar italipuka kwa
sababu ya Dr Shein kukataa matokeo ya uchaguzi?
Hatari kubwa zaidi kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla
ni vijana kuamini kuwa hatuwezi kuleta mabadiliko kwa njia za kidemokrasia.
Watu wenye itikadi kali zisizoamini mfumo wa demokrasia watapata mwanya wa
kuendeleza itikadi hizo na kupata wafuasi hasa vijana. Dr Shein jiulize unataka
kutupeleka huko?
Tuwashukuru na kuwapongeza Wazanzibari kwa kuendelea
kuwa watulivu na kuwa na matumaini ya kupatikana ufumbuzi wa haki. Lakini tuelewe
uvumilivu wa Wazanzibari una kikomo. Kutangaza rasmi kurudia uchaguzi kunaweza
kuwa chanzo cha vurugu za kisiasa zinazoweza kuleta maafa makubwa. Nani
atakayesimamia uchaguzi huo ikiwa taarifa ya Mwenyekiti wa ZEC kuwa wajumbe
wake wanadundana itakubaliwa kuwa ni ya kweli? Kama Tume na Sekretariati yake
imeharibu uchaguzi wa Oktoba 2015 watawezaje kusimamia uchaguzi mwingine? Kama
uchaguzi wa Zanzibar umeharibika kwa nini uchaguzi wa Wabunge na Rais wa
Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Zanzibar uhesabiwe kuwa ni halali wakati
ulifanyika siku moja kwa kutumia daftari la ZEC na vituo vya kupigia kura
vilivyoandaliwa na ZEC? Uchaguzi wa Zanzibar umekamilika. Matokeo yapo.
Mchakato wake ukamilishwe na yatangazwe.
Watanzania hasa viongozi wa dini na madhehebu
mbalimbali, viongozi wa asasi za kiraia, viongozi wastaafu, vyombo vya habari
na wapenda haki tusilifumbie macho tatizo la kisiasa la Zanzibar. Tumshauri Dr
Shein akubali mchakato wa kutangaza matokeo ukamilishwe. Ni aibu kuulizwa na
Marekani kuwa uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa shwari na wa amani kwanini matokeo
yake yamefutwa? Kama CCM aiheshimu maamuzi ya Wapiga kura wa Zanzibar
itaheshimu maamuzi ya Watanzania wote ikiwa itashindwa uchaguzi wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano?
Imetolewa na
Ibrahim Haruna Lipumba
Mwenyekiti Mstaafu

0 comments:
Post a Comment