![]() |
| Rais wa Rwanda Paul Kagame |
Rwanda haitatuma wanajeshi wake kwenye kikosi Umoja wa
Afrika cha ulinzi wa amani nchini Burundi. Hayo yamesemwa na Rais Paul Kagame
huku akikanusha madai kwamba nchi yake inawapa silaha na mafunzo wakimbizi kwa
ajili ya kufanya uasi nchini Burundi.
Mapema Ijumaa Umoja huo wenye wanachama 54 ulisema kuwa
ungetuma kikosi cha askari 5,000 kwa lengo la kukomesha gahsia zinazoibua
wasiwasi kuwa Burundi inarudi kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe. AU imeahidi
kutuma kikosi hicho licha ya Burundi kupinga kile ilichokiita kama “kikosi cha
uvamizi”.
Ghasia nchini humo zililipuka mwezi Aprili baada ya Rais
Pierre Nkurunziza kutangaza azma yake ya kugombea muhula wa tatu, ambao
alishinda katika uchaguzi uliofanyika mwezi Julai. Uhusiano baina ya Rwanda na
Burundi uko katika hali mbaya, ambapo Bujumbura inaituhumu Kigali kuwa
inawaunga mkono waasi wenye silaha na wapinzani wa kisiasa wa Rais Nkurunziza.
“Tumesema wazi kuwa hata kwenye kikosi hicho
kitakachotumwa Burundi, hatutashiriki,” Kagame aliwaambia wanahabari mapema Jumanne.
“Lakini tunaweza kutoa mchango wetu kwa namna tofauti,”
aliongeza bila kutoa maelezo ya kina.
Mamia ya watu wameuawa ndani ya miezi kadhaa ya
maandamano nchini humo, ambayo yamepelekea kuzuka kwa mashambulizi ya risasi
ambayo yamekuwa yakitokea hivi karibuni nyakati za usiku huku maiti za watu
zikionekana katika mitaa ya Bujumbura karibu kila siku.
“Jambo muhimu ninaloliona ni kupata jibu la namna
Burundi inavyoweza kusaidiwa kupata suluhisho la kisiasa,” Kagame alisema. “Kwa
awali halionekani kuwa tatizo la kijeshi, ingawa tunaona mambo mengi yanatokea
ambayo yanaweza kuhitaji matumizi ya kiwango fulani cha uingiliaji kati ili
kukomesha mauaji.”
Kagame alikanusha tuhuma zinazotolewa na maafisa wa
Burundi na mashirika ya misaada kwamba Rwanda inatoa mafunzo na silaha kwa
waasi.
Shirika la misaada kutoka nchini Marekani la Refugees
International wiki iliyopita lilisema kuwa wanaume na vijana katika kambi ya
Mahama iliyoko nchini Rwanda, ambayo inasimamiwa na Umoja wa Mataifa na
serikali ya Rwanda, wanapewa mafunzo ya kijeshi na kupewa vitisho pindi
wanapokataa.
Shirika hilo limesema kuwa vijana hao wa Kirundi hupewa
mafunzo nchini Rwanda na kisha juhudi hufanyika kuwatuma Burundi kupitia Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Kongo.
“Tumewaambia watu wafanye uchunguzi na kubaini nani
amekwenda wapi na kwa namna gani,” Kagame alisema.
“Sijaona ushahidi hata mdogo wa jambo hilo hivyo
linakuzwa kisiasa,” Kagame alisema na kuziita tuhuma hizo kuwa “za kitoto”.
Wasiwasi wa kimataifa unazidi kuongezeka juu ya kusambaa
kwa ghasia zinazoendelea nchini Burundi.

0 comments:
Post a Comment