Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa
wakilinda maeneo nyeti ya kiuchumi na kijamii Zanzibar tangu kufutwa matokeo ya
uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu, wameondolewa kuanzia juzi katika maeneo
hayo.
Askari hao walikuwa wameimarisha ulinzi katika Bandari
ya Malindi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kituo cha
Matangazo cha Televisheni na Radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC),
Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kiwanja cha Watoto
cha Michezo cha Kariakoo.
Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Kamishina wa
Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, alithibitisha askari wa JWTZ
kuondoka katika maeneo hayo na jukumu la ulinzi kuchukuliwa na polisi.
Alisema mahitaji ta askari yanapokuwa makubwa hasa
katika kipindi cha uchaguzi, katika
baadhi ya malindo hulazimika kuchukuliwa askari wa JWTZ kwa madhumuni ya kuimarisha usalama
zaidi katika maeneo hayo.
Alisema kutokana na hali ya Zanzibar kuwa shwari, askari
wa JWTZ wataendelea na majukumu yao mengine na askari polisi kurudi katika
malindo yao ya kawaida baada ya majukumu yao ya kazi kupungua tangu kufanyika
uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Kamishna Hamdan alisema wakati wa shughuli za kitaifa au
uchaguzi mkuu askari polisi wanakabiliwa na majukumu mengi ndiyo maana sehemu
ya majukumu ya kazi zao huchukuliwa na askari wa JWTZ kwa muda yakiwemo
malindo.
Hata hivyo, alisema pamoja na askari hao wa JWTZ
kuondolewa katika maeneo hayo, lakini Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi ya
Zanzibar (Zec) yataendelea kulindwa na
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment