![]() |
| Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi |
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, ametishia kupambana
na vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika vitakavyopelekwa nchini humo,
katika maelezo yanayoonekana kuwa yenye utata zaidi tangu kuzuka kwa mgogoro wa
kisiasa nchini mwake.
Mwezi huu, Umoja wa Afrika ulisema kuwa uko tayari
kutuma walinda amani 5,000 kwa lengo la kuwalinda raia waliojikuta katika miezi
kadhaa za ghasia, jambo lililopelekea kwa mara ya kwanza kwa umoja huo
kuingilia kijeshi dhidi ya utashi wa mwanachama wake.
“Kila mtu anapaswa kuheshimu mipaka ya Burundi,” Nkurunziza
alisema katika maelezo yake kwenye kituo cha radio cha serikali.
“Iwapo watakiuka misingi hiyo, watakuwa wameishambulia
nchi na kila raia wa Burundi atasimama na kupambana nao… nchi itakuwa
imeshambuliwa na itajibu mapigo,” alisema katika jibu lake la kwanza la wazi
dhidi ya mpango huo wa AU.
Maafisa wengine wa serikali wameshasema kuwa vikosi
vyovyote vya walinda amani vitakavyoingia bila idhini ya Burundi vitakuwa
vimekwenda kinyume na mamlaka ya nchi hiyo.
Zaidi ya watu 220,000 wameikimbia nchi hiyo tangu mgogro
huo ulipolipuka mwezi Aprili kutokana na uamuzi wa Rais Nkurunziza kugombea
muhula wa tatu.
Makundi ya upinzani yaliingia barabarani kwa madai kuwa
hatua hiyo inakiuka katiba. Lakini alishinda kesi ya kikatiba na hivyo kugombea
katika uchaguzi uliofanyika mwezi Julai ambao alishinda.
Mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli, kuendelea kwa ghasia na
mashambulizi ya silaha yameibua wasiwasi katika ukanda huu ambao bado una
kumbukumbu ya mauaji ya kimbari yaliyotokea nchini Rwanda mwaka 1994 na ambayo
vidonda vyake bado havijapona.

0 comments:
Post a Comment