![]() |
| Ufaransa imeongeza sheria ya dharura kutoka siku 12 hadi miezi 3 kufuatia vitisho vya kiusalama baada ya mashambulizi ya Paris. |
Ufaransa yumkini ikaifunga misikiti ipatayo 160 katika
kipindi cha miezi kadhaa ijayo kama sehemu ya operesheni ya kitaifa ya jeshi la
polisi chini ya hali ya dharura inayoruhusu maeneo ya ibada yanayoeneza
mitazamo mikali kufungwa, mmoja wa maimam wakubwa amesema.
Kufuatia taarifa kwamba misikiti mitatu imeshafungwa tangu
mashambulizi ya Novemba 3 kwenye mji wa Paris, Hassan El Alaoui, ambaye ni
mas-uli wa kuteua maimamu wa kimkoa na kieneo na ambaye ni mtu wa kati baina ya
maimamu na maafisa wa magereza, aliiambia Al Jazeera jana Jumatano kuwa
misikiti mingi imepangwa kufungwa.
"Kwa
mujibu wa takwimu rasimu na majadiliano yetu na wizara ya mambo ya ndani, baina
ya misikiti 100 na 160 itafungwa kwa sababu inaendeshwa kinyume na sheria na
bila vibali sahihi, au inatumia mahubiri ya kuwakufurisha Waislamu wengine,”
alisema.
"Aina
hii ya mahubiri yasingepaswa kuruhusiwa katika nchi za Kiislamu, achilia mbali
nchi zenye usalama kama Ufaransa,” alisema El Alaoui.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ya hivi karibuni ya kuifunga misikiti,
ilifanywa chini ya “mamlaka ya kesheria” na ilitakiwa iwe imefanyika kwa sababu
ya “baadhi ya mambo yanayokiuka sheria waliyoyakuta”.
El Alaoui
anasema kuwa Ufaransa kuna jumla ya misikiti 2,600.
Sheria ya dharura iliyoongezwa na Ufaransa imekuwa ikihusisha
ukamataji, uvamizi wa makazi na mali binafsi kufuatia mashambulizi ya Paris –
ikiwa ni pamoja na kuvamia misikiti na biashara zinazomilikiwa na Waislamu – na
imeibua wasiwasi miongoni mwa mashirika ya haki za binadamu kwamba sheria hiyo
inaweza kubana na kwenda kinyume na uhuru wa watu.
Wakati
huo huo, kuna wasiwasi kwamba jamii ya Waislamu nchini humo inakabiliwa na
ongezeko la manyanyaso kutokana na baadhi ya watu kushindwa kutofautisha baina
ya Waislamu na wale wanashirikiana au kuunga mkono makundi ya wanamgambo kama
vile kundi la Dola la Kiislamu katika Iraq na Sham (ISIL) ambalo limedai
kuhusika na shambulizi hilo lililotokea Novemba 13.
"Kuwa Muislamu nchini Ufaransa sio jambo rahisi, ni hali
ngumu,” anakiri Felix Marquardt, Muislamu anayeishi Paris na muasisi
mwenza wa taasisi ya al-Kawakibi Foundation na kuongeza: "hususan wanawake wanaovaa hijabu, ni
waathirika wa ubaguzi, na kwa wanaume inakuwa ngumu kupata kazi”.
Marquardt
anasema kuongezeka kwa chuki dhidi ya Uislamu kufuatia mashambulizi hayo sio
jambo la kushangaza ingawa halieleweki.
"Uhusiano
baina ya watu wanaofanya matendo ya kinyama duniani ni kwamba wanadhani kuwa
wao wenyewe ni Waislamu. Madamu Waislamu wanakataa kulitazama hilo kwa makini…
ninadhani ni jambo hatari kitaaluma na kimaadili na hali mbaya itazidi
kujitokea.”
CHANZO: Al Jazeera
![France extended emergency laws from 12 days to three months amid increased security threats following the Paris attacks [Getty]](http://www.aljazeera.com/mritems/imagecache/mbdxxlarge/mritems/Images/2015/11/29/50c14556fb05480f827883bf42fd773e_18.jpg)
0 comments:
Post a Comment