KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM), Nape Nnauye amepata ajali mbaya akiwa njiani kuelekea Lindi akitokea
jijini Dar es Salaam.
Nape amenusurika kifo katika ajali hiyo iliyotokea leo
asubuhi katika eneo la Njia Nne Kilwa akiwa anatoka Dar kuelekea jimboni kwake.
Nape ambaye pia ni mgombea Ubunge wa Jimbo la Mtama,
Lindi alipata ajali hiyo baada ya tairi la mbele la gari aliyokuwa akiendesha
aina ya Toyota Land Cruiser kupasuka na kupinduka mara kadhaa katika eneo la
Nyangao mkoani Lindi.
Katika gari hilo, Nape alikuwa peke yake na ndiye
alikuwa akiendesha gari hilo ambapo amepata majeraha madogo ila anaendelea
vizuri.
Akizungumza na mtandao huu, Nape amesema:
"Namshukuru Mungu nimetoka salama na nawaomba wananchi wasiwe na hofu japo
ajali ilikuwa mbaya maana gari lilipinduka mara kadhaa, nimepata majeraha
madogomadogo na michubuko ila ni mzima.
Gari limeharibika vibaya ila ninachoshukuru nilikuwa
nimefunga mkanda na 'air bag' nazo zimenisaidia."
Kabla ya ajali hiyo, Nape alikuwa jijini Dar es Salaam
ambapo aliungana na mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dk. John Pombe Magufuli
aliyekuwa na mikutano kadhaa ya kampeni katika jiji la Dar na baada ya shughuli
hiyo alikuwa akirejea Lindi kuendelea na kampeni kwenye jimbo lake la Mtama.



0 comments:
Post a Comment