
HATUWEZI KUSHINDA UBUNGE SEGEREA
Ndugu zangu, kwa moyo mkunjufu kabisa napenda
kuwajulisha kuwa hatuwezi tena kushinda ubunge wa jimbo hili kwenye uchaguzi
uliofanyika jana.
Matokeo ya majumuisho ya kila kata yanaonesha kuwa
mgombea wa Chadema, Bi. Anatropia Theonest ana wastani wa kura 2000 - 2500 kwa
kila kata.
Mimi nina wastani wa kura 4000 - 5000 kwa kata na
mgombea wa CCM ana wastani wa kura 5000 hadi 6000 kwa kata.
Hii ina maana kuwa kura za UKAWA kama zingelipigwa kwa
mgombea halisi wa UKAWA tungeishinda CCM kwa zaidi ya kura 20,000 lakini kwa
sababu zimepigwa kwenda vyama viwili tunaweza kushindwa kwa wastani wa kura
5000 hadi 10,000.
Haya yaliyotokea hapa Segerea ni funzo kubwa kwa vyama
vyetu na wanasiasa wetu kuheshimu na kusimamia makubaliano, kuwa na roho ya
kufikiria mustakabali wa taasisi na watu wetu kuliko MASLAHI BINAFSI. Kwa hatua
ya sasa sitaeleza hujuma za ndani kwa ndani tulizofanyiana ndani ya UKAWA hadi
kufika hapa.
Nachoweza kusema ni Asante Mungu na asante wana Segerea,
asante watu wote waliojitoa kufa na kupona kutusaidia, lakini pia asante kwa
wale wote waliotusaliti kimya kimya ili kuchochea mgawanyiko wa kura hizi.
Naahidi kushiriki katika hatua zote za kumsaidia mshindi
wa uchaguzi wetu ili atangazwe rasmi kuwa mbunge wa wana Segerea. Mimi
nitaendelea na majukumu mengine lukuki ya kulijenga taifa letu.
Kwa sababu yaliyosababisha kukosa ushindi wetu ni mambo
ya ndani ya vyama vyetu, sitachukua hatua zozote wala kukata rufaa kwa sababu
wananchi hawakutunyima ushindi, tumeugawanya wenyewe.
Nawapongeza madiwani wa UKAWA walioshinda kwenye kata
zote 13 za jimbo letu, tulishirikiana na kupambana pamoja hadi kuleta ushindi
huu, nawataka wachape kazi kufa na kupona na waisimamie manispaa ya Ilala bila
woga, nawaomba wakatumie mipango na ushauri tuliowahi kupanga pamoja ili
kuwatendea wana Segerea yale waliyoyatarajia.
Mwisho, nataka kuwaeleza watanzania wote kuwa sina
kinyongo na mtu yeyote kwa matokeo haya. Mimi ni kati ya watu wanaoamini kuwa
SIASA SI AJIRA...Nitaendelea kuwatumikia watanzania kwa njia zote muhimu nje ya
vyombo vya maamuzi.
Nataka kuwaambia wananchi wa Segerea kwamba niko imara
sana, sijayumba wala kutetereka, nawapenda sana nyote na poleni na MSHTUKO wa
matokeo haya na muda si mrefu tutayaweka hapa.
Ni mimi,
Mtatiro Julius,
Segerea.
0 comments:
Post a Comment