
TAARIFA YA CHAMA CHA MAPINDUZI
CCM inapenda kutoa taarifa ifuatayo kwa wana-CCM na kwa
umma:
MALALAMIKO YA CCM KUHUSU MATOKEO KWENYE BAADHI YA
MAJIMBO
Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa
kukusanya na kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne
kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika kujumlisha
matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.
Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe.
Wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na
utata uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba kura
zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko kwenye sheria.
Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani
walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua kwenda
mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya.
Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi
umeheshimiwa. Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama
kulikuwa na ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura.
Hata hivyo, tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi
tulikopoteza viti vya Ubunge, tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko,
tunaheshimu maamuzi ya wananchi, na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili
tubaini makosa na kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi.
Tumefarijika kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu
ulikuwa wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba changamoto
zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache kiasi zisingeweza
kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.
Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali
kuhusu namna ya kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo
kuimarisha demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa
jinsi uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo sahihi
cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia
mkutano wao na waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba
hawakubali matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya
Ubunge wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea.
Tunashangazwa kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais
ni hiyo hiyo iliyoandaa uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni
vilevile, na sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo
walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika sehemu
(columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani.
Mawakala wao walisaini fomu hizo kwenye vituo vya kupiga
kura. Wameanza kuwa na matatizo na matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa
kushindwa. Kama mwelekeo ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume,
wasimamizi na taratibu zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga
demokrasia yetu na kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa
anayeshindwa kunyanyua simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza.
Nafasi ya mwisho aliyonayo Mgombea wa UKAWA kuendelea
kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa mwanademokrasia, ni kwa kufanya
hivyo siku Dkt. Magufuli atakapotangazwa mshindi.
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na
kutengeneza sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa
nchi, ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi
wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri sita
ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali. Nguvu na
utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni,
tutawapata madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape
nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za
kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za vurugu na
maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha wafuasi wa UKAWA
kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi.
Amani ya nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka
la mtu yoyote. Wenzetu wa UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya
kuiingiza nchi yetu machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani
wafanye vurugu na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za
watu wengine.
Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama
kawaida huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015
0 comments:
Post a Comment