Aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Juma Mwapachu leo
ametangaza kujivua uanachama wa chama hicho kutokana na chama kupoteza dira.
Tamko la Balozi Mwapachu ambalo Mwananchi imethibitisha
kutoka kwake linasema kuwa kuanzia kesho kada huyo wa CCM hatakuwa tena
mwanachama wa chama hicho tawala na kuongeza kuwa bado hajaamua kujiunga na
chama kingine.
‘’Kuanzia kesho
mimi si mwana CCM tena. Nitarejesha rasmi kadi yangu kupitia ofisi ya CCM ya
kata yangu Mikocheni, Dar es Salaam. Kwa sasa sijaamua kujiunga na chama
kingine. Mwenyezi Mungu anilinde,” inasema sehemu ya tamko hilo.
Mwanasiasa huyo ambaye amekuwa ndani ya CCM kwa miaka 48
sasa amesema kuwa katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa chama hicho,
chama kilidhihirisha kutokuwa chama kinachoendeshwa kwa misingi ya demokrasia
kwa kumuengua waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ambaye anapendwa na wengi
ndani ya chama.
Mwapachu amesema kuwa Lowassa na wanachama wengine wa
CCM waliojitoa ni sahihi hivyo naye anaungana nao.
‘’Kujitoa kwake
uanachama wa CCM hivi karibuni ni sahihi kabisa kwasababu CCM si chama tena cha
watu. Kimetekwa, na mimi nakubaliana na msimamo wa Lowassa na hao waliyofuata
kutoka ndani ya CCM,’’ alisema Mwapachu.
Mwapachu ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama
hicho lakini pia amewahi kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
CHANZO: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment