![]() |
| Askofu Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba. |
·
Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu, hatimaye Askofu
Msaidizi Methodius Kilaini wa Jimbo Katoliki la Bukoba ameibuka na kutoa sifa
za rais chaguo la Mungu kutoka katika orodha ya wagombea nane wa nafasi hiyo
wakiwamo Dk. John Magufuli wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza katika mahojiano maalum na Nipashe mwishoni
mwa wiki, Askofu Kilaini anayekumbukwa zaidi kwa madai kuwa ndiye aliyemtabiria
Rais Jakaya Kikwete, kuwa Rais baada ya kumtaja ndiye chaguo la Mungu katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, alisema rais ajaye baada ya Uchaguzi Mkuu Oktoba
25, anapaswa kuwa na walau sifa nane muhimu ili akidhi kigezo cha kuliongoza
taifa hili vizuri na kwa mafanikio.
Mosi, Askofu Kilaini aliitaja sifa ya uadilifu, akisema
ni muhimu kwa kila mgombea anayepaswa kuliongoza taifa hili baada ya uchaguzi
mkuu mwezi ujao.
Askofu Kilaini aliitaja sifa ya pili kuwa ni 'kuchapa
kazi kwa vitendo'. Alisema sifa hii pia ni muhimu kwa Rais ajaye kwani
atalazimika kuonyesha kwa vitendo katika kuchapa kazi na siyo kinyume chake.
Sifa ya tatu kwa rais chaguo la Mungu, kwa mujibu wa
Askofu Kilaini, ni kwa mgombea atakayekuwa akitekeleza majukumu yake ipasavyo
huku sifa ya nne ikiwa ni hali ya kuwa na uzalendo wa kweli, kwa kufanya kila
jambo kwa maslahi ya taifa.
Sifa ya tano kwa rais anayepaswa kuongoza taifa hili ni
kuwa mchamungu, sifa ya sita kuwa ni mpenda watu huku ya saba, kwa mujibu wa
Kilaini, ni kuwa mtu asiye bosi kwa wananchi bali mtumishi wao (wananchi).
"Sifa nyingine (ya nane) ni ujasiri wa kuweza
kuwakemea wale wote wasio waadilifu (katika serikali yake)," alisema
Askofu Kilaini.
Alipotakiwa amtaje kwa jina mgombea anayetimiza vigezo
hivyo vya kuwa "Chaguo la Mungu", Askofu Kilaini alisema hawezi
kufanya hivyo sasa na badala yake anasubiri uchaguzi ukishafanyika kwani
anaamini kuwa nguvu ya Mwenyezi Mungu ni kubwa na kwa vyovyote vile, kiongozi
ajaye (rais) atapatikana kwa nguvu yake (Mungu).
Mbali na Magufuli na Lowassa anayewakilisha pia vyama
vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, NLD, NCCR-Mageuzi
na Chama cha Wananchi (CUF), wagombea wengine wa urais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ni Chifu Lutasola Yemba wa ADC, Janken Kasambala wa NRA, Fahmy
Dovutwa wa UPDP, Anna Mghwira wa ACT-Wazalendo, Hashim Rungwe wa Chaumma na
Maximilian Lymo wa TLP.
ATOA MAZITO
Katika hatua nyingine, Askofu Kilaini amewataka Dk.
Magufuli, Lowassa na wagombea wengine wa urais kuwakumbusha watu wao kuwa
wazingatie kuiweka mbele amani ya nchi kwani uchaguzi ukimalizika maisha
yataendelea kama kawaida.
“Ninalowaasa Watanzania wasipoteze fursa hii ya
kuwasikiliza wagombea. Watu wafurahi, uchaguzi si vita si, watu kuchukiana, uwe wakati wa kufurahi licha
ya kuwapo mapungufu madogo... lazima tulinde amani yetu kwani mara baada ya
uchaguzi maisha yataendelea,” alisema Askofu Kilaini.
Hata hivyo, Kilaini alisema kuwa anachofarijika ni kuona
kuwa hadi sasa kampeni kuelekea uchaguzi mkuu zinaendelea kufanyika kwa amani
na kwamba, hadi sasa hakuna tukio kubwa la kuogofya kiasi cha kutishia amani ya
taifa.
“Angalau kwa wagombea wakubwa (wa nafasi za urais), bado
hatujapata kitu kibaya kama kuhamasisha watu wachaguane kwa dini, ukabila na
ukanda. Hilo linakatazwa kwenye katiba yetu na sisi viongozi (wa dini) hatuwezi
kuacha kulikemea hilo kila wakati linapojitokeza... daima tunapaswa
kuwakumbusha watu kuwa siasa si mahala pa udini, ukanda na wala si mahala pa
ukabila," alisema Askofu Kilaini.
Aidha, aliongeza kuwa ni wajibu pia kwa viongozi wa dini
wakiwamo wa kanisa lake (Katoliki) kuhakikisha kuwa wanawahamasisha watu
kujitokeza kwenye kampeni, kusikiliza ahadi za wagombea na vyama vyao na
mwishowe kujitokeza siku ya kupiga kura ili kuwachagua watu wanaoamini kuwa
wanafaa kuongoza.
“Ninalowaasa Watanzania ni kwamba wasipoteze fursa hii
(ya mikutano ya kampeni). Wajitokeze kuwasikiliza wagombea na kuchambua ilani
na ahadi wanazotoa kabla ya kufanya uamuzi siku ya kupiga kura," alisema.
DINI NA SIASA
Kilaini alisema miongoni mwa kasoro chache
zilizojitokeza hadi sasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi ni kuwapo
kwa baadhi ya viongozi wa dini wanaoonekana kuchanganya siasa na dini, ingawa
hilo halijaleta athari kubwa hadi kufikia sasa.
Alisema yeye na viongozi wengine wa dini hawaachi
kukumbushana juu ya wajibu wao katika kipindi hiki ambao ni pamoja na
kutoonyesha ukereketwa kwa chama au kwa mgombea yeyote na pia kuwatayarisha
watu ili wapige kura kwa haki, amani na uhuru.
Alisema hivi karibuni, viongozi wa dini nchini
walikutana na maafisa wa serikali wakiwamo Mkuu wa Jeshi la Polisi, Msajili wa
Vyama vya Siasa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kujadili mambo
mbalimbali kuhusiana na uchaguzi na mwishowe walikubaliana kuwa wao (viongozi
wa dini) wasionyeshe ukereketwa wa vyama wala wagombea binafsi na kamwe sehemu
za ibada zisitumike kwa kampeini za siasa.
Alisema nafasi ya kanisa lao (Katoliki) kwa uchaguzi
wowote ule ukiwamo wa Tanzania ni kuhamasisha watu wawe na uhuru wa kuchagua
mtu wamtakaye, kuhamasisha haki itendeke ili kila mmoja aridhike na matokeo na
pia, kuhamasisha amani ambayo ni tunu muhimu kwa taifa.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment