![]() |
| Waandamanaji katika mji mkuu wa Burkina Faso, Ouagadougou jana Septemba 21, 2015. |
Wakuu wa kijeshi nchini Burkina Faso wamewaamuru askari
wa kikosi cha ulinzi wa rais, kilichofanya mapinduzi dhidi ya serikali ya mpito
wiki iliyopita, kuweka silaha zao chini.
Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, wakuu hao wa
kijeshi wamewatolea wito wanamapinduzi hao kuzisalimisha silaha zao kwenye
kambi za jeshi kwa ahadi ya kudhamini usalama wao.
Wamesema kuwa vikosi vya taifa hilo vinaelekea katika
mji mkuu, Ouagadougou, kutoka mikoani kwenda kuwanyang’anya silaha askari wa
kikosi cha ulinzi wa rais bila kumwaga damu.
"Vikosi vyote vya taifa vinaelekea Ouagadougou kwa
lengo moja la kuwapokonya silaha kikosi cha ulinzi wa rais (RSP) bila kumwaga
damu,” ilisema taarifa hiyo na kuongeza, "Tunawataka wajisalimishe."
Mapinduzi hayo yalifanywa na Jenerali Gilbert Diendere, mshirika
wa karibu wa aliyekuwa Rais Blaise Compaore, ambaye aliondolewa madarakani mwaka
jana kufuatia maandamano ya kuipinga serikali yake baada ya kutaka kufanya jaribio
la kubadili katiba ili kubaki madarakani.
Viongozi wa mapinduzi mapya wametangaza kulivunja bunge
na serikali ya mpito ambayo ilipewa jukumu la kuongoza kipindi cha mpito baada
ya kung’olewa kwa Compaore mwaka jana.
Jenerali Diendere ametawazwa kuwa kiongozi mpya wa Burkina
Faso licha ya hatua hiyo kulaaniwa vikali na nchi za Magharibi na Umoja wa
Afrika (AU).
Serikali ya mpito iliyokuwa ikiongozwa na Kafando
ilikuwa imepanga tarehe 11 Oktoba kuwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa rais na
wabunge, ambao ungekuwa wa kwanza tangu Compaore alipoondolewa madarakani.
Kwa uchache watu 10 wamepoteza maisha na wengine kadhaa
kujeruhiwa katika mfululizo wa ghasia tangu yalipofanyika mapinduzi hayo.

0 comments:
Post a Comment