MAMLAKA ya Kudhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA), imesitisha kwa muda usiojulikana leseni ya usafirishaji abiria ya
kampuni ya mabasi ya Muro (Muro Investment Co. Limited), kwa kutokidhi viwango
vya kiufundi na usalama.
Aidha, Sumatra imeiagiza kampuni hiyo kuwasilisha kwa
mamlaka hiyo mpango wa utengenezaji magari yake, nakala ya cheti cha ofisa
usafirishaji wa kampuni pamoja na mkataba wake wa ajira, iweze kujiridhisha
endapo matakwa ya kanuni za ufundi, ubora na usalama yamezingatiwa na kutimizwa.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Gilliard
Ngewe, kampuni hiyo ilijulishwa kuhusu uamuzi huo ambao utekelezaji wake
unaanza leo kwa mabasi yote ya Muro yanayosafirisha abiria kutoka Dar es
Salaam- Arusha na Dar es Salaam- Mwanza.
Kufuatia maelezo ya Ngewe, mabasi hayo yamekuwa
yakilalamikiwa na abiria kwa kuharibika mara kwa mara pindi yawapo safarini,
hivyo kushindwa kutoa huduma ya usafiri kwa viwango vinavyotakiwa.
Alisema, “Inapotokea mabasi yanayosafirisha abiria
yanapata hitilafu za mara kwa mara na kushindwa kuwapa abiria mabasi mbadala
wakamilishe safari zao, mamlaka inawajibika kufanya uchunguzi na kuchukua hatua
stahiki, ikiwa ni pamoja na kusitisha leseni ya usafiri kwa kampuni husika”.
Mkurugenzi Mkuu huyo alisema, hatua iliyochukuliwa dhidi
ya kampuni ya Muro ilizingatia ushahidi uliotolewa na abiria waliofikisha
malalamiko yao kwa mamlaka hiyo, wakiwemo walioachwa wakihangaika njiani
Septemba 17, mwaka huu, kwa zaidi ya saa 15 bila kupatiwa suluhisho wala huduma
za kibinadamu.
Inaelezwa abiria hao walikuwa wakisafiri kwa basi la
Muro lenye namba za usaji T51BQP, kutoka Dar es Salaam kwenda Arusha,
lililoharibika katika eneo la Chalinze mkoani Pwani saa 3:00 asubuhi hadi saa
6:30 usiku, bila wahusika kuwaeleza abiria chochote.
Mamlaka hiyo pia ilieleza kuwa, abiria wa mabasi hayo
yaendayo Mwanza yakitokea Dar es Salaam wamekuwa wakikutwa na kadhia ya aina
hiyo wawapo safarini, ambapo mara kwa mara wamejikuta wakihangaika njiani pindi
yanapoharibika bila kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Ngewe alitaja mabasi mengine ambayo yanahusika na adhabu
hiyo kuwa ni lenye namba za usajili T780BPY lililoharibika Septemba 5, mwaka
huu katika eneo la Ruvu Darajani mkoani Pwani na T788BPY lililoharibika Septemba
11, mwaka huu katika eneo la Mailimoja-Kibaha mkoani humo.
Mabasi mengine yaliyofungiwa ni yenye namba za usajili;
T 881 BUR, T 485 BQV, T 536 CYC, T 540 CYC, T 534 CYC, T 531 CYC. “Makosa
yaliyofanywa na kampuni ya Muro ni ukiukwaji wa kanuni namba 21 na 22 ya Kanuni
za Leseni za usafirishaji kwa magari ya abiria ya mwaka 2007 na Kanuni namba 11
ya (1)(b) ya viwango vya ubora na usalama vya mwaka 2008,” alisema.
Sumatra ilieleza kuwa kufunguliwa kwa leseni kwa kampuni
hiyo kutategemea majibu yatakayotolewa na mkaguzi wa magari kutoka jeshi la
Polisi, baada ya matengenezo yatakayofanywa katika magari hayo.
CHANZO: Hhabari Leo
0 comments:
Post a Comment