![]() |
Straika wa Tottenham Hotspur Emmanuel Adebayor wakati wa
mechi dhidi ya Stoke City kwenye uwanja wa White Hart Lane mjini London Desemba
22, 2012
|
Mshambuliaji wa Togo Emmanuel Adebayor amefunguliwa
mlango wa kuondoka Tottenham Hotspur kwa makubaliano yaliyofikiwa baina ya
pande mbili, klabu hiyo imetangaza leo.
Kuondoka kwa straika huyo mwenye umri wa miaka 31
kulitarajiwa baada ya kutojumuishwa katika kikosi cha wachezaji 25 wa Tottenham
katika Ligi Kuu msimu huu au kupewa namba.
"Tunaweza kuthibitisha kuwa tumefikia makubaliano
na Emmanuel Adebayor ambayo yatamruhusu kuondoka klabuni,” Spurs wamesema
katika taarifa iliyowekwa kwenye tovuti yao. “Tunamtakia Emmanuel kila la heri
katika mustakbali wake.”
Adebayor aliyewahi kuchezea klabu za Metz, Monaco, Arsenal,
Manchester City na Real Madrid, alijiunga Spurs kwa mkopo mwaka 2011, kisha
akasaini mkataba wa kudumu Agosti 2012.
Mwaka 2011 - 2012 alikuwa mfungaji bora wa Spurs akiwa
na magoli 18, lakini mwaka 2013 meneja Andre Villas-Boas alimwambia afanye
mazoezi na timu ya vijana ya klabu hiyo.
Kuteuliwa kwa Tim Sherwood kama mrithi wa Villas-Boas
kulimuibua tena Adebayor kwa muda mfupi, lakini alianza kutoonekana sana baada
ya Mauricio Pochettino kuchukua mikoba ya kuifundisha klabu hiyo msimu
uliopita, akionekana mara 10 tu.
"Nilikuwa muwazi kwake. Tulifanya mazungumzo kabla
ya msimu uliopita kufikia kikomo na nilimwelezea wazo langu,” Pochettino alisema
juzi Ijumaa.
"Nadhani iko wazi kuwa hayuko akilini mwangu au
katika mipango ya baadae ya Tottenham. Si tatizo kwake wala kwetu.
"Ilikuwa wazi tokea mwanzo, miezi mitatu au minne
iliyopita, na alikuwa na uamuzi wa kubaki au kuondoka.
"Muda wote tuko tayari kumsaidia. Tuna uhusiano
mzuri. Tatizo pekee kwa sasa ni kutafuta ufumbuzi kwake na kwa klabu, jambo
ambalo ni zuri kwa pande zote mbili.”

0 comments:
Post a Comment