![]() |
| Waziri Mkuu wa Misri Ibrahim Mahlab |
Serikali ya Waziri Mkuu wa Misri Ibrahim Mahlab imewasilisha
barua ya kujiuzulu katika ofisi ya rais wa nchi hiyo.
"Waziri mkuu amekabidhi barua ya kujiuzulu kwa
serikali yake kwa rais ambaye ameipokea,” ilisema taarifa iliyotolewa na ofisi
ya Rais wa Misri Abdel Fattah al-Sisi.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikufafanua zaidi sababu za
kujiuzulu kwa serikali hiyo.
Imeripotiwa kuwa Mahlab ameombwa kuhudumu kama waziri
mkuu wa mpito mpaka serikali mpya itakapoundwa. Sisi amemtaka waziri wa mafuta,
Sharif Ismail, kuunda serikali mpya ndani ya wiki moja.
![]() |
| Aliyekuwa Waziri wa Kilimo wa Misri Salah El Din Mahmoud Hilal |
Tukio hilo limekuja siku kadhaa baada ya waziri wa
kilimo Salah El Din Mahmoud Hilal kujiuzulu na kisha kutiwa nguvuni kwa tuhuma
za ufisadi.
Hayo yanatokea wakati watumishi wa sekta ya umma
wakipanga kufanya maandamano makubwa kupinga sheria ya utumishi wa umma yenye
utata, ambayo hivi karibuni ilipitishwa na Sisi. Waziri wa mambo ya ndani
ameapa kuzima maandamano hayo.
Misri ilikumbwa na ghasia tangu kupinduliwa kwa rais wa
kwanza kuchaguliwa kidemokrasia, Mohammed Mursi, katika mapinduzi ya kijeshi ya
mwezi Julai mwaka 2013 yaliyoungwa mkono na Sisi, ambaye wakati huo alikuwa
mkuu wa jeshi la nchi hiyo.
Baada ya mapinduzi hayo, maelfu ya wafuasi wa Mursi
waliwekwa korokoroni, wengi wao wakihukumiwa adhabu ya kifo akiwemo Mursi
mwenyewe.


0 comments:
Post a Comment