![]() |
(Kutoka
kushoto) Mawaziri wa Mambo ya nje wa Venezuela, Ecuador, Colombia na Uruguay,
Delcy Rodriguez, Ricardo Patino, Maria Angela Holguin na Rodolfo Nin Novoa wakihudhuria
mazungumzo katika mji mkuu wa Ecuador, Quito, Septemba 12, 2015.
|
Colombia na Venezuela zimekubaliana kufufua uhusiano wa
kidiplomasia uliovunjika baada ya mgogoro wa mipaka baina ya mataifa hayo
mawili ya Amerika ya Kusini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Colombia Maria Angela Holguin na
mwenzake wa Venezuela, Delcy Rodriguez, wamekutana katika mji mkuu wa Ecuador, Quito
hapo jana.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ecuador Ricardo Patino na
mwenzake wa Uruguay Rodolfo Nin Novoa, ambao serikali zao zimekuwa zikiwataka
maafisa wa Bogota na Caracas kumaliza tofauti zao, walihudhuria pia.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja iliyosomwa na Patino, wanadiplomasia
hao waandamizi kutoka Colombia na Venezuela walipiga “hatua ya kuridhisha”
katika kushughulikia “masuala nyeti”, na watashauriana na viongozi wao kuhusu
mipango ya kuwakutanisha marais wao kutatua kukamilifu mgogoro huo wa mipaka.
Mkutano wa awali baina ya Holguin na Rodriguez uliofanyika
Agosti 26 haukuzaa matunda.
![]() |
Raia wa Venezuela
wakirudi kutoka Colombia wakiwa wamekwama mpakani katika eneo la Paraguachon katika
jimbo la Venezuela la Zulia, Septemba 10, 2015.
|
Bogota na Caracas zimekuwa katika mgogoro tangu mwezi
jana, baada ya Rais wa Venezuela Nicolas Maduro kufung sehemu ya mpaka wa nchi
hizo.
Uamuzi huo ulikuja baada ya askari watatu wa Venezuela
kushambuliwa na watu wenye silaha wakati wakifanya operesheni dhidi ya magendo
katika mji wa San Antonio katika jimbo la Tachira Aprili 19.
Mataifa hayo yaliwaita mabalozi wao kufuatia mzozo huo,
jambo lililosababisha kufukuzwa kwa kiasi cha raia 1,500 wa Colombia wanaoishi Venezuela.
Mpaka huo wenye urefu wa kilometa 2,200 (maili 1,400) ni
eneo lenye msitu mkubwa ambapo shughuli nyingi za magendo na biashara haramu
hufanyika.


0 comments:
Post a Comment