Rais Jakaya Kikwete amesema anashangazwa na Mwanasheria
wa Chadema, Tundu Lissu kumtaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mwenye
Richmond yupo na anatembea naye mikoani.
Kikwete aliyasema hayo jana wakati akiwaaga wananchi wa
Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na kumtaka Lissu amtaje mwenye
Richmond.
“Endapo Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond,
nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe,” alisema Kikwete.
Kabla ya mkutano huo, Rais Kikwete alifungua jengo la
Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) ambalo limejengwa kwa Sh7 bilioni.
Akifungua jengo hilo, aliwaomba wawekezaji na mifuko ya
kijamii kuiga mfano wa NSSF kwa kuwekeza katika sekta ya majengo kwa kuwa
yanapendezesha mji.
Kadhalika, Rais Kikwete alizindua jengo la Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na nyumba 36 za bei nafuu zilizopo katika eneo la
Mlole, Kigoma Mjini.
RICHMOND
Suala la Richmond imekuwa moja ya ajenda za CCM katika
kampeni za urais hasa baada ya Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa
aliyejiuzulu wadhifa huyo kwa kashfa hiyo kuhamia upinzani.
Kila sehemu ambako mgombea urais wa CCM anakwenda, suala
hilo limekuwa likiibuliwa, huku Lowassa akisema yeye hakuhusika, bali
alijiuzulu kuiokoa Serikali isianguke kwa kuwa ulikuwa uamuzi wa wakubwa.
Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amekuwa akienda
mbali zaidi akisema akichaguliwa ataanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia
mafisadi wanaosababisha umaskini nchini.
CHANZO: Mwananchi

0 comments:
Post a Comment