![]() |
| Ndege ya Urusi ikipakua shehena mjini Latakia, Syria, Septemba 12, 2015. |
Maafisa wa Marekani wamefichua kuwa Urusi inatumia anga
ya Iran na Iraq kupeleka zana za kijeshi na askari nchini Syria, na hivyo
kuongeza mvutano baina yake na Marekani.
Kwa mujibu wa ripoti moja, kwa uchache ndege kubwa za
usafirishaji wa zana za kijeshi aina ya Antonov An-124 ziliondoka kutoka kambi
moja nchini Urusi wiki moja iliyopita kwa lengo la kupeleka zana za kijeshi
nchini Syria kwa kutumia anga za Iran na Iraq, gazeti la New York Times limeripoti
leo Jumatatu kwa kuwanukuu maafisa wa Marekani.
Maafisa hao wameliambia gazeti hilo kuwa ndege hizo
zimetua katika uwanja mmoja wa ndege katika jimbo la Latakia magharibi mwa
Syria.
Kwa mujibu wa taarifa za kintelejensia za Marekani, meli
za kijeshi na makombora ya Urusi vinaulinda uwanja huo wa kijeshi huko Latakia.
Kwa kutumia njia mpya ya anga, Moscow inapuuza juhudi za
Washington kuzuia usafirishaji huo na jambo hilo linaongeza mvutano baina ya
mataifa hayo.
Awali ikulu ya Marekani ilikuwa na matarajio kuwa
imezuia harakati za Urusi kupeleka zana za kivita na wanajeshi nchini Syria
baada ya Bulgaria ambayo ni mwanachama wa NATO kutangaza kuwa usingeruhusu anga
yake kutumiwa na Urusi.
Lakini kwa haraka sana, Urusi ilianza kurusha ndege zake
kuelekea Iran na Iraq, huku Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, Sergey Lavrov,
akisema jana Jumapili kuwa wataendelea kufanya hivyo licha ya upinzani wa
Marekani.
“Usafirishaji wa zana za kijeshi ulikuwepo, unafanyika
na utaendelea kufanyika,” alisema bwana Lavrov kama alivyonukuliwa na mashirika
ya habari ya Urusi. “Zana hizo zinasindikizwa na wataalamu wa Urusi, ambao
husaidia kuziandaa, kuwapa mafunzo askari wa Syria namna ya kuzitumia.”
Lavrov aliongeza kuwa Moscow itaendelea kuipa silaha
serikali ya Syria katika vita vyake dhidi ya wanamgambo wa kundi la Dola ya
Kiislamu, akizitaka nchi nyingine kuchukua msimamo kama huo na kuisaidia
Damascus katika vita hivyo.
Utawala wa Obama umeionya Moscow na kuitaka iweke ukomo
wa usafirishaji wa zana za kijeshi nchini Syria.
Juzi Jumamosi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani,
John Kerry, alimpigia simu Lavrov na kuonya kwamba Washington ina wasiwasi
mkubwa kuhusu ripoti za Urusi kujijenga kijeshi katika eneo hilo.
Migogoro iliyotokea katika mataifa ya Syria na Ukraine
yameibua mvutano baina ya Urusi na mataifa ya Magharibi. Moscow na Washington zimekuwa
na tofauti kubwa kuhusu migogoro ya Syria na Ukraine.
Syria ilitumbukia katika machafuko tangu mwezi Machi
mwaka 2011. Maelfu ya raia wamepoteza maisha huku wengine milioni 10 wakiwa
ukimbizini.

0 comments:
Post a Comment