NJAMA ZA KUIHUJUMU UKAWA JIMBO LA SEGEREA HAZITAFANIKIWA!!
Nimeshuhudia mimi mwenyewe jana usiku gari la Matangazo
likipita Vingunguti kuhujumu uzinduzi wa kampeni za UKAWA jimbo la Segerea. Na
anayefanya hivyo ni mwenzangu dada Anatropia Theonest wa CHADEMA. Ameibuka tena
na kutangaza kuwa anazindua kampeni za CHADEMA katika kata ya Liwiti leo kwa
muda na wakati ambapo UKAWA kwa ujumla inazindua kampeni kuninadi.
Ikumbukwe kuwa dada yetu huyu tayari amepewa barua rasmi
na Katibu Mkuu wa CHADEMA na kujulishwa kuwa mgombea rasmi wa UKAWA ni Julius
Mtatiro (mimi) na aniunge mkono. Na hata baada ya kupewa barua ile alinipongeza
na kusisitiza kuwa tutashirikiana kuiondoa CCM madarakani na pongezi zake
niliziweka hadharani pia.
Nataka kuwahakikishia wananchi wa Segerea kuwa uzinduzi
wetu wa UKAWA uko palepale, ni LEO JUMAPILI kuanzia saa 7 hadi saa 12 jioni,
viwanja vya Vingunguti Relini. Madiwani wote wa UKAWA watakuwa hapa Vingunguti
na hata viongozi wote wa CHADEMA ngazi ya matawi, kata, jimbo, mkoa na taifa
watakuwa hapa Vingunguti.
Kwa sababu vurugu hizi anazifanya hadharani na naambiwa
anatangaza kuwa ni bora jimbo liende CCM kuliko CUF kuongoza, nataka yeye na
watu wachache wenye mtizamo huo wajue kuwa UKAWA imejipanga na inaangalia
maslahi mapana ya Segerea na Taifa. Nataka nimwambie mwenzangu kuwa mimi, UKAWA
na wananchi wa Segerea tumepanga kushinda uchaguzi wa mwaka huu na tutapigana
pamoja na kushinda na hata yeye akiendelea kutupinga, anajua matokeo yake ni
nini.
Nimekaa kimya muda mrefu na sikutaka kumueleza jambo
hata alivyokiuka maamuzi ya viongozi wakuu wa UKAWA ya mgao wa jimbo hili,
wakati huo alijenga hoja kuwa hajapata barua rasmi kutoka kwenye chama chake,
chama chake kimemuandikia barua kutoka makao makuu/Katibu Mkuu - akaipokea,
akaikubali na kunipongeza, siku moja mbele amebadilika, anasema barua ile ni
FEKI. Barua ambayo CHADEMA wameipeleka ngazi zote kuanzia kanda, mkoa na wilaya
hadi jimbo.
Tayari nafanya kazi na wagombea udiwani wote wa CHADEMA
jimbo la Segerea na wale wa CUF pia, sisi tuendelee na kazi na tumpe dada yetu
muda atafakari hili vurugu analoanzisha lina maslahi ya nani! Ukawa? Segerea?
Taifa? Chadema? Binafsi? Wapambe? CCM? au maslahi ya nani.
UKAWA jimbo la Segerea tumejipanga kushinda, na
tutashinda kwa kishindo. Na dada yetu akijirudi na kuunga mkono MABADILIKO
tutampokea, asiporudi kundini tutamtakia kila la heri kwenye kampeni zake.
Mtatiro, J,
Segerea - Dar es Salaam,
06 Septemba 2015.



0 comments:
Post a Comment