![]() |
| Wanamgambo wa Al-Shabab nchini Somalia |
Kundi la wanamgambo wa al-Shabab limeutwaa mji mwingine
katika eneo la katikati mwa Somalia baada ya vikosi vya Umoja wa Afrika
(AMISOM) kuondoka katika eneo hilo.
“Leo tumeuchukua mji wa Buqda kwa amani. Mji huo sasa
upo chini ya udhibiti wetu,” msemaji wa kundi hilo, Sheikh Abdiasis Abu Musab,
amesema.
Vikosi vya AMISOM, ambavyo viliudhibiti mji huo kutoka
kwa wanamgambo hao mwezi mmoja uliopita, viliondoka katika mji huo Jumamosi
usiku. Ahmed Nur, afisa mwandamizi wa jeshi la Somalia, amesema kuwa askari
wameondoka katika mji huo kwenda kupambana na al-Shabab katika maeneo mengine,
na kwamba watarudi.
Huu ni mji wa tatu kuangukia mikononi mwa wanamgambo hao
tangu siku ya Ijumaa.
Ndani ya siku tatu zilizopita wanamgambo hao wameitwaa
miji ya El Saliindi, kilometa 65 (maili 40) kusini mwa mji mkuu, Mogadishu, na
mji wa Kuntuwarey, ulio baina ya Mogadishu na bandari ya Barawe, yote ikiwa
katika jimbo la Shabelle ya Chini.
Kundi hilo ambalo linalenga kuiangusha serikali ya
Somalia, hufanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya maafisa wa serikali na
walinda amani wa AMISOM nchini humo.
Mapema Jumamosi, wanamgambo hao waliushambulia msafara
wa AMISOM nje ya mji wa Marka na kusababisha vifo.
Somalia imekuwa katika ghasia baina ya vikosi vya serikali
na wanamgambo wa al-Shabab tangu mwaka 2006.
Mwaka 2011, wanamgambo hao waliondolewa mjini Mogadishu
na miji mingine mikubwa nchini humo katika makabiliano yaliyoendeshwa na vikosi
vya serikali kwa kushirikiana na vikosi vya AMISOM vinavyoundwa na askari
kutoka Uganda, Ethiopia, Burundi, Djibouti, Kenya na Sierra Leone.

0 comments:
Post a Comment