![]() |
| Rais wa Guatemala Otto Perez |
Rais wa Guatemala amezuiliwa na mahakama kuondoka nchini
mwake kufuatia fukuto la kashfa ya ufisadi wa mamilioni ya dola iliyoukumba
utawala wake.
Ofisi ya mwendesha mashitaka iliiomba mahakama kumzuia
Rais Otto Perez na mahakama ililikubali ombi hilo.
Hukumu hiyo imetolewa saa chache baada ya bunge la nchi
hiyo kupiga kura kwa wingi kumuondolea kinga rais huyo na hivyo kumfanya aweze
kushitakiwa.
Anatuhumiwa kuhusika na mpango ambao wafanyabiashara
wataweza kutoa hongo kukwepa ushuru wa forodha.
Mwendesha mashitaka Thelma Aldana amesema kuwa rais Perez
anachunguzwa kutokana na uwezekano mkubwa wa kuhusika na hongo na ukwepaji wa
ushuru wa forodha.
"Guatemala inaonesha kuwa hakuna aliye juu ya
sheria, na huu ni ujumbe wa watumishi wa umma wa sasa na wa baadaye kwamba
mienendo yetu lazima iendane na mamlaka ya katiba”, amesema.
Aidha, msemaji wa Rais amesema kuwa rais huyo anautambua
mchezo huo, ambao si mzuri ingawa kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kutokea, na
kuongeza kuwa ataheshimu utawala wa sheria.
Makamu Rais wa zamani wa nchi hiyo Roxana Baldetti, ambaye
msaidizi wake binafsi alitajwa kuongoza kashfa hiyo, na idadi kadhaa ya
mawaziri, wameshajiuzulu kutokana na sakata hilo.

0 comments:
Post a Comment