![]() |
| Dk James Mataragio |
KARIBU nusu ya eneo la Tanzania, imetajwa kuwa na miamba
inayohifadhi rasilimali muhimu ya kiuchumi ya mafuta na gesi, ambalo bado
halijafanyiwa utafiti.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC), Dk James Mataragio, aliyasema hayo hivi karibuni katika Jiji
la San Antonio nchini Marekani, iliposhiriki katika moja ya mikutano mikubwa
duniani, inayojumuisha washiriki na wadau wa kimataifa wa mafuta na gesi.
Mkutano huo pia uliambatana na maonesho ya kimataifa.
Kutokana na fursa hiyo, amesema TPDC iko mbioni kufanya
utafiti wa kitaalamu uitwao “Airborne Gravity Gradiometer Survey” katika maeneo
ya nchi kavu Kusini-Mashariki mwa Pwani ya Tanzania na upande wa Mashariki mwa
Bonde la Ufa.
Utafiti huo kwa mujibu wa Dk Mataragio, unatarajiwa
kuanza mwezi huu na utasaidia kuongeza thamani ya maeneo hayo kwa kutambua
maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuhifadhi rasilimali za mafuta na gesi na
utajumuisha eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 30,000.
Mbali na utafiti, pia amesema TPDC, inaendelea
kutekeleza dhima yake ya kukuza uwekezaji katika sekta hiyo ya mafuta na gesi.
“Katika kipindi hiki ambapo bado hali ya sekta ya mafuta
na gesi iko chini kutokana na kushuka kwa bei ya mafuta, ni muhimu sana kwa
nchi kama zetu ambazo bado zina fursa nyingi za utafiti wa mafuta na gesi,
kujitangaza zaidi ili kuvutia wawekezaji wakubwa,” alisema.
Mkurugenzi wa shughuli za mkondo wa chini, Dk Wellington
Hudson alisema; “Mkutano huu umelenga kuangalia teknolojia mpya ya kutafuta
mafuta na gesi ambayo ni tofauti na teknolojia ile ya kawaida. “Wenzetu wa
Marekani ndio nchi pekee iliyoweza kuzalisha rasilimali hizi zijulikanazo kama
unconventional resources,” alisema.
Teknolojia hiyo ni inayoruhusu kutafuta mafuta na gesi
katika miamba ambayo kwa njia ya kawaida ya utafiti isingewezekana kuzalisha.
CHANZO: Habari Leo

0 comments:
Post a Comment